Usafiri wa SGR Morogoro – Dodoma kuanza leo

January 3, 2026 11:57 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Uhakiki  wa usalama wa miundombinu ya reli watajwa kuwa chanzo cha kusitishwa kwa safari hizo.

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kurejea kwa usafiri wa treni ya mwendo kasi (SGR) leo jioni, baada ya kusitishwa kwa muda safari kati ya Morogoro na Dodoma kufuatia uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua kubwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 2, 2025 na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbalawa wakati akizungumza na Wananchi wa Gulwe wilayani Mpwapwa alieleza kuwa kusitishwa kwa safari hizo kulilenga kutoa nafasi ya kufanya uhakiki wa usalama wa miundombinu ya reli.

Taarifa hii inakuja ikiwa ni siku mbili toka kusitishwe kwa safari hiyo kutokana na athari za mvua zilizopelekea uharibifu wa miundombinu katika eneo la Kidete (Kilosa, Morogoro) na Godegode (Mpwapwa, Dodoma).

Kufuatia athari hiyo, safari zote za SGR zilikuwa kati ya Dar es Salaam – Morogoro na Morogoro – Dar es salaam suala lililokwamisha shughuli mbalimbali ikiwemo za kibiashara.

Aidha, kulingana na Waziri huyo, eneo la Kidete lilipata changamoto ndogo katika tuta la reli, na mafundi wameendelea na matengenezo ambayo yako katika hatua za mwisho. 

“Naomba niwahakikishie, tatizo lililojitokeza kwenye mradi wa SGR halitajitokeza tena Mungu akipenda,” ameeleza Waziri Mbalawa.

Huenda matengenezo hayo yakatatua ama kumaliza kabisa hitilafu zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara katika usafiri wa SGR mwanzoni mwa Novemba hadi Desemba 2025.

Pamoja na matengenezo hayo Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba hivi karibuni alisema kusitishwa kwa safari za SGR kupisha matengenezo ni utaratibu wa kawaida ambao unafanyika duniani kote.

“Hata mashirika makubwa ya ndege ya nchi zilizoendelea ikitokea mvua yenye upepo wanahairisha safari…

…Mimi niwaambie TRC maisha ya Watanzania ni kipaumbele cha kwanza usalama wao ni kipaumbele cha kwanza bora mtu safari yake iahirishwe asafiri muda ambapo tuna uhakika atafika salama,” alieleza Waziri Mkuu Nchemba jana  Januari 2, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks