TRA kuzindua mfumo mpya wa kodi utakaotumia AI 

January 5, 2026 6:32 pm · Goodluck Gustaph
Share
Tweet
Copy Link
  • Mfumo huo unatarajiwa kuongeza ufanisi, uwazi na kupunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.

Dar es Salaam: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kuzindua mfumo mpya wa kodi unaotumia teknolojia ya akili bandia (AI) ujulikanao kama Integrated Domestic Revenue Administration System (IDRAS), kwa lengo la kuboresha usimamizi wa kodi na kurahisisha huduma kwa walipakodi.

Hayo yamebainishwa leo Januari 5, 2026 na Kamishina Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda katika mkutano wa tathmini ya utendaji kazi wa TRA kwa nusu ya mwaka wa fedha 2025/2026, uliofanyika jijini Arusha.

Akizungumza katika mkutano huo, Kamishna Mwenda amesema mfumo huo mpya utafanyika kwa njia ya mtandao hivyo utapunguza ulazima wa walipakodi kufika ofisini mara kwa mara.

“Mfumo wa IDRAS utaondoa changamoto ya wafanyabiashara kukutana mara kwa mara na maafisa wa TRA, kwani huduma nyingi zitapatikana mtandaoni, lengo ni kuwapa wafanyabiashara muda zaidi wa kuendesha shughuli zao badala ya kuja ofisini kwetu,” amesema Kamishna Mwenda.

Aidha, amebainisha kuwa mfumo huo utatumia teknolojia ya akili bandia(AI) kufanya uchambuzi wa taarifa za kodi, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi, uwazi na kupunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo ameitaka TRA kuendelea kuimarisha mifumo yake ya Tehama kwa kujilinganisha na nchi nyingine zilizopiga hatua kiteknolojia.

“Tujipime na nchi ambazo zimeshatutangulia, tujiulize tutawafikiaje. Itakapofika wakati ambapo taarifa zote za mlipa kodi zinapatikana kwa urahisi na kwa wakati, ufanisi wa mamlaka ya mapato utaongezeka kwa kiasi kikubwa. Hivyo bado kuna haja ya kuendelea kuimarisha mifumo yetu,” amesema Waziri Khamis.

Uzinduzi wa mfumo wa IDRAS unaashiria hatua kubwa ya TRA katika mageuzi ya kidijitali ya ukusanyaji wa kodi nchini yakilenga kupunguza gharama za uendeshaji na kuimarisha mazingira rafiki kwa walipa kodi, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks