Upotevu wa chakula unavyochangia baa la njaa duniani
- Asilimia 13 za chakula hupotea kabla hazijawafikia walaji
- Asilimia 17 za chakula hutupwa majumbani, sehemu za kuuza chakula na kwenye masoko ya chakula
- Fao yaja na teknolojia kukabiliana na upotevu wa chakula
Dar es Salaam. Wakati baadhi ya maeneo duniani yanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, imebainika kuwa kiasi kikubwa cha chakula kinachozalishwa hakiwafikii watumiaji kutokana na kupotea wakati wa uvunaji, kabla na baada ya kufika sokoni.
Takwimu mpya zilizotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (Fao) zinaonyesha mwaka 2022 asilimia 13 za chakula zilipotea baada ya kuvunwa na kabla ya kufika sokoni.
Takwimu hizo zinabainisha kuwa zaidi ya asilimia 17 za chakula zilitupwa majumbani, sehemu za utoaji huduma za chakula na kwenye masoko ya chakula.
Mpaka sasa takribani watu milioni 783 duniani kote wanakabiliwa na njaa huku watu 25,000 ikiwemo watoto 1,000 wakipoteza maisha kila siku, kutokana na kukosa chakula.
Zinazohusiana : Afrika inavyoweza kukabiliana na baa la njaa
QU Dongyu Mkurugenzi Mkuu wa Fao, aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya uhamasishaji wa upotevu wa chakula na taka Septemba 30,2023 jijini Rome nchini Italia, amebainisha kuwa kupunguza upotevu wa chakula kukuwa msaada mkubwa wa kuimarisha usalama wa chakula duniani.
“Kupunguza upotevu wa chakula na taka kunatoa ushindi katika mambo matatu …usalama wa chakula, mabadiliko ya hali ya hewa, na kuongezeka kwa upatikanaji wa chakula chenye lishe bora huku ikiboresha mifumo ya chakula na kilimo,” amesema Qu.
Mbali na upotevu wa chakula Fao, inasema tatizo la njaa husababishwa na kupanda kwa bei za vyakula, pembejeo za kilimo na nishati kulikosababishwa na athari za vita vya Ukraine pamoja na ukosefu wa ajira,ambapo nchi za Afrika ni wahanga wakubwa.

Teknolojia kupunguza upotevu wa chakula
Katika kutambua mchango wa teknolojia katika kupunguza upotevu na uharibifu wa chakula FAO imezindua program tumizi (App) inayoitwa FLAPP itakayozuia upotevu wa chakula.
Programu hii itaruhusu wadau wa chakula kupata taarifa kutoka kwa wakulima ili kuelewa vyema sehemu ambayo upotevu wa chakula hutokea katika mnyororo wa thamani wa chakula kuanzia uzalishaji mpaka kinnamfikia mlaji.
Ili kutumia programu hiyo utalazimika kuwa na intaneti na kujisajili ili kupata taarifa utakazozihitaji.
Latest
