Kwa undani: Faida Vodacom Tanzania yapaa, M-Pesa, data kileleni
- Faida baada ya kodi ya Vodacom Tanzania yafikia Sh107.1 bilioni ikiwa ni kiwango cha juu kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka saba.
Dar es Salaam. Licha ya uwekezaji mkubwa katika uboreshaji wa miundombinu, Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC imepata faida baada ya kodi ya Sh107.1 bilioni katika mwaka ulioishia Machi, 2026, kiwango cha juu zaidi kurekodiwa ndani ya miaka saba.
Faida hiyo iliyoongezeka kwa asilimia 18 kutoka Sh90.5 bilioni iliyoripotiwa mwaka ulioishia Machi 2025, ni mwendelezo wa hatua za Vodacom kuimarisha uendeshaji wa biashara baada ya kuripoti hasara ya Sh30.1 bilioni mwaka 2021.
Hii ina maana kuwa Vodacom imeongeza faida baada ya kodi kwa zaidi ya Sh16.6 bilioni ndani ya mwaka mmoja.
Ripoti ya awali ya kifedha kwa mwaka ulioishia Machi 31, 2026 ya Vodacom Tanzania inaeleza kuwa utendaji huo mzuri ulichochewa zaidi na kukua kwa mapato ya huduma pamoja na jitihada za kupiga panga matumizi katika kampuni hiyo.
Vodacom Tanzania, kampuni pekee ya mawasiliano iliyoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ilirekodi mapato ya Sh1.88 trilioni katika mwaka unaoishia Machi 31, 2026 kutoka mapato ya Sh1.54 trilioni yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka jana, sawa na ukuaji wa takriban asilimia 22%.
Sehemu kubwa au zaidi ya theluthi mbili (asilimia 68) ya mapato hayo ya Vodacom yamechangiwa na mapato kutoka kwenye M-Pesa na huduma za intaneti (data), na kuvifanya kuwa ni vyanzo vikubwa vinavyoiingizia mapato mengi kampuni hiyo. Mapato ya data na M-Pesa kwa jumla yalikuwa ni Sh1.28 trilioni katika kipindi hicho.
Uchambuzi zaidi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa mapato ya Sh734.8 bilioni kutoka M-Pesa inayotoa huduma za kifedha kwa njia ya simu ni makubwa kuliko mapato ya mwaka ya baadhi ya benki za biashara nchini. Vodacom ni miongoni mwa kampuni chache nchini ambazo mapato yake ya mwaka yamevuka zaidi ya Sh1 trilioni.

M-Pesa, intaneti vyaendelea kukimbiza
M-Pesa ni miongoni mwa huduma za kibunifu nchini zilizochochea kwa kiwango kikubwa ujumuishi wa kifedha Tanzania kupitia simu za mkononi kwa huduma zake za msingi za zile ziada kama utoaji mikopo kwa wajasiriamali, bima na usimamizi wa fedha wa vikundi vya kijamii kupitia M-Koba.
Uchambuzi wa ripoti hiyo unabainisha kuwa amana kupitia huduma ya M-Koba inayoendeshwa kwa ushirikiano na Benki ya biashara ya Tanzania Commercial Bank (TCB) ziliongezeka kwa asilimia 80% katika mwaka unaoishia Machi 31, 2026 huku thamani ya amana kwa mwaka ikivuka Sh1 trilioni.
Zaidi ya asilimia 60 ya thamani ya amana zilizofanywa kwenye M-Koba, kwa mujibu wa Vodacom, zilifanywa na wanawake, jambo linaloonyesha kukubalika kwa huduma hiyo na mchango wake katika kuwawezesha kiuchumi watumiaji wake.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire amesema katika ripoti hiyo kuwa utendaji wa malengo ya biashara ya kampuni hiyo ulikuwa wa kuridhisha na faida ya mwaka huo iliathiriwa na ongezeko la muda la gharama zilizotokana na mpango wa uboreshaji wa mtandao.
“Bila kuhesabu athari za gharama hizi za ziada za mara moja, faida yetu ya msingi baada ya kodi ilikuwa TZS204.1 bilioni, zaidi ya mara mbili ya kiasi kilichorekodiwa mwaka uliopita. Utendaji huu uliimarishwa na ukuaji mkubwa wa mapato ya huduma, pamoja na mikakati ya kuokoa gharama iliyotumika katika mwaka huo,” anaeleza Besiimire.

Miongoni mwa maeneo ambayo Vodacom ilipunguza matumizi ni kwenye gharama za kukodi minara na matengenezo ambapo waliokoa zaidi ya Sh1 bilioni moja ndani ya mwaka mmoja. Matumizi ya kukodi minara na matengenezo yameshuka hadi Sh149.4 bilioni kutoka Sh150.5 bilioni yaliyoripotiwa kwa mwaka ulioishia Machi 2025.
Zaidi ya Sh300 bilioni zatumika kuboresha mtandao
Katika mwaka wa fedha ulioishia Machi 2026, Vodacom walitumia Sh323.9 bilioni katika matumizi ya kimtaji kwa ajili ya kupanua na kuboresha mtandao na kuimarisha mifumo ya Tehama ili kuhimili ongezeko la mahitaji, na kuboresha uzoefu wa wateja katika hatua inayofuata ya ukuaji.
“Uwekezaji huo unaweka msingi thabiti wa mafanikio endelevu ya kibiashara, ukisaidia uchakataji wa miamala kwa haraka na salama zaidi, pamoja na ukuaji wa idadi ya wateja,” anasema bosi huyo wa Vodacom Tanzania.
Matokeo hayo ya kifedha yanakuja wakati Vodacom Tanzania inasheherekea maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake ikiwa na wateja zaidi ya milioni 33.4 hadi kufikia Machi 2026, kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Ongezeko hilo la faida ni neema kwa wawekezaji wa kampuni hiyo wakiwemo Watanzania takriban 40,000 waliowekeza kupitia DSE ambao mwaka huu walishuhudia hisa za kampuni hiyo zikiongezeka thamani hadi Sh1,000 kwa hisa moja mwanzoni mwa mwaka huu kabla ya kushuka kidogo. Hadi soko la hisa linavyofungwa leo (Mei 14, 2026) hisa moja ya Vodacom ilikuwa ikiuzwa wastani Sh780 kwa hisa.
Latest