Wasiwasi watanda kushambuliwa mtambo wa nyuklia Ukraine
- Ni mapigano makali yanayoendelea karibu na mtambo huo.
- Wataalam waonya athari zitakazotokea endapo utashambuliwa.
- Wataka ulindwe kwa mujibu wa kanuni za kimataifa.
Dar es Salaam. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejulishwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa ripoti za mapigano makali kwenye maeneo yanayozunguka mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia nchini Ukraine, mtambo ambao ni mkubwa zaidi barani Ulaya.
Mkuu wa Idara ya masuala ya siasa wa Umoja wa Mataifa, Rosemary Dicarlo amesema hayo Machi 4, 2022 akihutubia Baraza hilo lililokutana kufuatia ombi la Ukraine baada ya majeshi ya Urusi kurusha makombora kwenye jengo jirani na mtambo huo wa nyuklia.
Dicarlo amesema operesheni za kijeshi katika maeneo ya nyuklia na maeneo ya raia siyo tu hayakubaliki bali pia ni ukosefu mkubwa wa uwabijikaji.
Amesema kila juhudi zinapaswa kuchukuliwa kuepusha janga la nyuklia kama ilivyokuwa kwenye mtambo wa Chernobly mwaka 1968 huku akipongeza juhudi za shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, (IAEA) kufuatilia hali ya usalama kwenye mtambo huo.
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi akihutubia wajumbe wa Baraza hilo amethibitisha kuwa operesheni katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia zinaendelea kama kawaida licha ya mashambulizi.
“Wadau wa Ukraine waliijulisha IAEA kuwa kombora lililorushwa usiku wa jana (Machi 3) lilipiga jengo kwenye moja ya vinu vya mtambo huo na kusababisha moto ambao hata hivyo baadaye ulizimwa,” amefafanua Grossi.
Soma zaidi:
- Baraza Kuu la UN laitaka Urusi iondoke Ukraine bila masharti
- UN yakwaa kisiki kuiwajibisha Urusi uvamizi Ukraine
- ICC yaelekeza macho yake Ukraine, Urusi ikiendelea na mashambulizi
IAEA inaendelea na mawasiliano na mamlaka za Ukraine, ikiwemo serikali na zile zinazosimamia usalama wa nyuklia pamoja kampuni inayoendesha mtambo huo, mawasiliano ambayo ndiyo msingi wa taarifa zote tunazoendelea kuhusu hali ya usalama.
Grossi ameeleza utayari wake wa kwenda Ukraine ili kushauriana na mamlaka husika pamoja na jeshi linalodhibiti mtambo huo ili kuhakikisha vigezo vya usalama vinazingatiwa akiongeza kuwa wanaamini kuwa wana wajibu wa kuitikia ombi la Ukraina la kusaidiwa katika kusimamia usalama wa mtambo huo.
Dicarlo amekumbusha kuwa mashambulizi dhidi ya mitambo ya nyuklia ni kinyume na sheria za kibinadamu za kimataifa.
Ibara ya 56 ya Itifaki ya Nyongeza ya Mkataba wa Geneva, inasema kuwa “kazi au mitambo yenye vitu vyenye nguvu kubwa kama vile mabwawa, vituo vya mitambo ya nyuklia haipaswa kushambuliwa hata kama maeneo hayo yanatumika kijeshi au mashambulizi ya aina hiyo yanaweza kusababisha madhara makubwa miongoni mwa raia.”
Kutokana na madhara yanayoweza kutokea endapo mtambo huo hautasimamiwa vizuri, Guterres ameitaka IAEA kufanya kila linalowezekana kudhibiti madhara yanayoweza kutokea.
Latest