UN: Watoto milioni 78 duniani kote hawaendi shule
Wanafunzi wawili wadogo huko Bol, Chad wakionyesha kazi yao kwenye ubao mweusi shuleni. Picha | UNICEF/Frank Dejongh.
- Ni kutokana na mapigano, mizozo, majanga ya tabianchi na ukimbizi.
- UN yataka hatua za haraka zichukuliwe.
Dar es Salaam. Watoto wa kike na wa kiume milioni 78 duniani kote hawaendi shuleni kabisa kutokana na mapigano, mizozo, majanga ya tabianchi na ukimbizi amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Guterres amesema hakuna mtu anapaswa kunyimwa fursa ya kujifunza.
Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia kwa njia ya video mkutano wa kusaka Dola za Marekani milioni 222 (Sh519.2 bilioni) kusaidia elimu kwa watoto walio kwenye majanga na mizozo ulioandaliwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kusongesha elimu kwenye maeneo ya majanga na mizozo ya muda mrefu (ECW).
Amesema kwa ujumla watoto milioni 222 million leo hii wanapata elimu isiyo na umakini.
“Haijalishi uko wapi, haijalishi unaishi wapi na wala vikwazo unavyokumbana navyo, ni lazima upate elimu bora,” amesema Guaterres jana akitoa wito wa juhudi zaidi za kimataifa kuhakikisha watoto wengi zaidi walio hatarini na wengineo wanapata fursa ya kuelimika.
Tangu mfuko huo uliopoanzishwa mwaka 2017, walimu 87,000 wamepatiwa mafunzo na kupatiwa watoto milioni 7 wanaoishi kwenye maeneo ya majanga elimu wanayostahili.
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu Duniani na pia Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu la ECW, Gordon Brown ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwezesha fursa ya kusoma kwa wote akisema ni uwekezaji wa amani endelevu.
“Tunazungumzia kuhusu watoto walio pembezoni zaidi, walio hohehahe na waliosahaulika zaidi duniani. Tunazungumzia kuhusu watoto wa kike ambao wanajikuta wakisafirishwa kiharamu au wakitumikishwa kwenye ajira au kulazimishwa kuolewa iwapo hatutawasaidia,” amesema Brown.
“Fedha zinazochangishwa hapa zipelekwe pia kwa nchi zinazopokea wakimbizi ili ziweze kutoa huduma inayotakiwa,” amesema Neema Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Tanzania ambaye pia ni mwakilishi wa Afrika katika mtandao wa wabunge vinara wa elimu duniani.
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kutoka Geneva, Uswisi kunakofanyika mkutano huo, Lugangira amesema “jambo kubwa lazima kusisitiza ni kwamba mara nyingi inapofanyika michango ya fedha kama hizo, unakuta nchi ambazo zinapokea wakimbizi na kuwapatia huduma mbali mbali huwa zinasahaulika.
“Kwa hiyo nikiwa natoka Tanzania na kwa niaba ya mataifa mengine ya Afrika niko hapa kusisitiza umuhimu wa kukumbuka nchi kama Tanzania ili ziweze kuendelea kutoa misaada mbalimbali lakini ziweze kuwa nyumbani kwa wenzetu wanapopata changamoto mbalimbali.”
Latest