Maziwa ya kopo: Kikwazo cha unyonyeshaji kinachohatarisha afya za watoto

February 25, 2022 12:08 pm · Herimina
Share
Tweet
Copy Link


  • Asilimia 41 pekee ya watoto waliopo chini ya miezi sita ndiyo hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee.
  • Ongezeko la matumizi ya maziwa ya kopo wachangia kushuka kwa unyonyeshaji.
  • WHO, UNICEF waonya kampuni za maziwa ya watoto kuzingatia maadili na miongozo.

Dar es Salaam. Maziwa ya mama ni moja ya njia salama ya ukuaji wa mtoto kwa sababu yana kingamwili ambazo zinasaidia kumlinda mtoto dhidi ya magonjwa mbalimbali ya utotoni.

Hata hivyo, uuzaji holela wa maziwa mbadala kwa ajili ya watoto, umezidi kudidimiza jitihada za unyonyeshaji watoto maziwa ya mama duniani.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shirika la kuhudumia watoto (UNICEF) inabainisha kuwa watoto wawili kati ya watatu  hawanyonyweshwi kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo, hali ambayo haijabadilika kwa miaka 20 iliyopita. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa watoto watatu kati ya watano hawanyonyeshwi katika saa za mwanzo baada ya kuzaliwa, huku asilimia 41 pekee ya watoto waiopo chini ya miezi sita ndiyo hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee.

Moja ya sababu ya hali hiyo iliyotajwa na mashirika hayo, ni pamoja na ushawishi wa kibiashara unaofanywa na makampuni ya maziwa ya viwandani, ambayo mengi yanakiuka viwango vya kimataifa vya ulishaji watoto wachanga.

Uchunguzi uliofanywa na WHO pamoja na UNICEF kwa wazazi 8,500, wanawake wajawazito na wahudumu wa afya 300 duniani kote, umegundua kuwa ushawishi wa uuzaji wa maziwa ya viwandani ulifikia zaidi ya asilimia 80 na kuongeza uwezekano wa wazazi kuchagua ulishaji watoto wao kwa maziwa ya kopo au ya viwandani.

“Ujumbe wa uwongo na wa kupotosha kuhusu maziwa ya unga ni kikwazo kikubwa kwa unyonyeshaji, unyonyeshaji ambao tunajua ni bora kwa watoto wachanga na akina mama,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell. 


Zinazohusiana


UNICEF na WHO zinaeleza kuwa tasnia ya maziwa ya viwandani yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 55 sawa na Sh127.4 trilioni  inatumia mikakati ya kimasoko na isiyo ya kimaadili ili kushawishi maamuzi ya wazazi ya ulishaji watoto wachanga na mila za kinyonyaji zinazohatarisha lishe ya watoto na kukiuka ahadi za kimataifa.

“Ripoti hii inaonesha kwa uwazi kwamba uuzaji wa maziwa ya kopo bado unaenea kwa njia isiyokubalika, ya kupotosha na ya fujo,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus baada ya ripoti hiyo kutolewa jana Februari 23, 2022.

Unyonyeshaji maziwa ya mama, humsaidia mtoto kuwa na uwezo mzuri wa kiakili, kupunguza uwezekano wa kupata maradhi kama kisukari anapokuwa wakubwa pamoja na kuwa na unene uliopitiliza.

WHO inabainisha kuwa zaidi ya watoto 820,000 duniani wangeokolewa kwa mwaka endapo watoto wenye miezi 0 hadi 23 wangenyonyeshwa maziwa ya mama  ipasavyo.

Ripoti hiyo imezitaka Serikali, wahudumu wa afya na tasnia nzima inayohusika na vyakula vya watoto kutekeleza kikamilifu na kutii mahitaji ya kanuni za kiafya ili kuokoa watoto.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW