Umachinga ulivyomsotesha mjasiriamali kukuza biashara kwa miaka 20

February 16, 2023 7:10 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Eliaika Mtui, mkazi wa jiji la Dar es Salaam ambaye bado hajaonja mafanikio ya biashara yake.
  • Asimulia jinsi mgambo na rushwa vilivyomkwamisha. 
  • Serikali yasema mzizi wa yote ni elimu ya mitaji na mikopo

Dar es Salaam. Ni miaka 20 ya kuhama hama, kukimbizana na kusaka senti kwa kuuza bidhaa unaomuwezesha kuendesha maisha ya familia.

Si jua wala mvua vilivyoacha kumsulubu akiwa sokoni kutafuta angalau chakula cha mtoto wake aliyempata mwaka mmoja tu mara baada ya kujiajiri mwenyewe kupitia ujasiriamali.

Ni Eliaika Mtui, mkazi wa jiji la Dar es Salaam ambaye kwa miaka 20 amekuwa akifanya biashara ya kuuza nguo za mtumba, ndala na viatu kwa kuhama hama akitafuta mahali pa kujikimu kuendeleza biashara yake yenye mtaji mdogo.

“Yaani ni kukimbizana,  mfano nilianzia Manzese, wakatuhamishia Urafiki, huko Urafiki  mpaka utengeneze eneo la biashara unakuta  kale ka mtaji kameisha,” anasema Mtui.

Hali hiyo imemfanya mama huyo anayeishi mwenyewe (single mother) kutopata mafanikio makubwa katika biashara yake,  zaidi ya kupata hela ya kula, kumsomesha mtoto wake na kujenga nyumba ndogo ya kuishi.

“Ndani ya miaka yote hiyo ya kufanya biashara nimefanikiwa kumsomesha mtoto wangu chuo kikuu bila mkopo na kujenga nyumba ambayo tunaishi sasa hivi,” anasema Eliaika. 

Eliaika Mtui (Kushoto) akizungumza na Afisa Biashara kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Judith Matage. Picha | Lucy Samson.

Eliaika bado anaona hayo ni mafanikio madogo, alitamani awe mbali zaidi lakini uelewa mdogo wa masuala ya biashara ndiyo umekuwa kikuzwa kikubwa kutoka katika mkwamo huo. 

Tangu aanze biashara mtaji wake haujawahi kuzidi Sh150,000 huku akitaja  kusumbuliwa na mgambo ambao wamekuwa wakiwaondoa katika maeneo ambayo anadai hayaruhusiwi kufanya biashara nako kumechangia kumpunguzia kasi ya kutulia na kujenga biashara yake.

“Usipowapa chochote hao mgambo au hao waonajiita viongozi wa wamachinga wanachukua vitu vyako na kwenda kuvikomboa ni lazima uwape hela,” anasema Eliaika.

Ukosefu wa maeneo ya kufanyia biashara ya uhakika na kodi ambazo zimekuwa zikiwaathiri wafanyabiashara wadogo hasa wanawake.

“Kwa siku unakuta naingiza Sh15,000 hapo niigawe Sh10,000 akiba na Sh5,000 hela ya kula, sasa  nitapata wapi hela ya kulipia meza ili nifanye biashara?,” amehoji mama huyo.

Eliaika anawakilisha kudni kubwa la wafanyabiashara wadogo wadogo au maarufu kama machinga wanaopitia wakati mgumu kufanya biashara zao kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya sehemu  za kufanyia biashara hizo.

Mara nyingine wafanyabiashara hao huambulia kufukuzwa na kuhamishwa kwa maeneo yao ya biashara kutokana na kanuni mbalimbali zinazopitishwa na Serikali.

Mathalan, mwaka 2022 wamachinga walipangwa upya na kuondolewa barabarani na kupelekwa katika maeneo maalum hasa masokoni ambako baadhi wanalalamikia uchache wa miundombinu na kukosa wateja. 


Soma zaidi


Nini kifanyike kuinua biashara za wanawake?

Baadhi ya wadau wa biashara waliohudhuria mdahalo wa wanawake katika sekta isiyo rasmi, ulioandaliwa na taasisi ya Policy Forum leo Januari 27, 2023 wametoa maoni mbalimbali yaliyolenga kuboresha ustawi wa wanawake kwenye sekta hiyo.

Msafiri Mariam, mfanyabiashara na mwanaharakati wa masuala ya wanawake na watoto anasema jambo linalokandamiza ustawi wa sekta isiyo rasmi hasa wamachinga ni uongozi mbovu wa kundi hilo.

Mwanaharakati huyo anatolea mfano viongozi hewa wa wamachinga wanaojichagua, kujipa madaraka na kutumia madaraka hayo kujipa maeneo ambayo yalitakiwa yawe ya wafanyabiashara hao.

“Shida ya viongozi hao ni kutokubali kutoka kwenye madaraka yao, tangu walipochaguliwa mpaka leo na wengine wanatumiwa na baadhi ya viongozi wa Serikali kujipatia maeneo ya biashara,” anasema Msafiri.

Mdau huyo anadai sababu nyingine ni kukosekana kwa usawa utoaji wa mikopo ya halmashauri inayotolewa kwa ajili ya vijana, wanawake na walemavu, jambo linalochangia baadhi ya biashara kuendela kudumaa.

Naye Irene Kanyakole kutoka Shirika la HakiElimu anasema mgawanyo usio sawa kwenye ugawaji wa vizimba vya biashara kati ya wanawake na wanaume ni jambo linaloridisha nyuma maendeleo ya sekta isiyo rasmi kwa wanawake.

Hali hiyo inasababisha baadhi ya wanawake kutoboa mifuko yao zaidi kupangisha meza na maneno ya kufanyia biashara ambayo yalitakiwa kugawiwa kwa usawa.

“Tunachosisitiza Serikali iwasajili wafanyabiashara wadogo, wajue wako wangapi ili hata wakati wa kugawa visimba wajue wamewafikia watu halisi na sio wafanyabiashara wakubwa au vigogo,” anasema Kanyakole.

Jopo la watoa mada kwenye mdahalo wa wanawake katika sekta isiyo rasmi (kushoto Eliaika Mtui, Judith Matage, Dominic Ndunguru na Iman Hatibu. Picha | Lucy Samson.

Serikali yatoa neno

Afisa Biashara kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Judith Matage anasema chanzo kikubwa cha kutoendelea kwa biashara zinazoendeshwa na wanawake ni kukosekana kwa elimu ya mitaji na  mikopo zinazotolewa na Serikali.

“Kila halmashauri huwa inatenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya mikopo ya vijana na wakina mama lakini si wengi wanaojitokeza kuchukua,” anasema Matage.

Kwa mujibu wa Afisa huyo Mwaka  2022/2023 Serikali ilitenga Sh600  milioni kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali, ikatenga tena  Sh45 bilioni kwaajili ya kujenga miundombinu na kuwawezesha wamachinga na Sh700 milioni kwa ajili ya kutoa maarifa kwa viongozi wa wamachinga.

Mbali na kuwepo kwa fursa hiyo ya mikopo afisa huyo amewataka wajasiriamali kuhamia maeneo waliyopangiwa na Serikali na kutoa taarifa endapo unyanyasaji na vitendo vyovyote viovu vinavyotendeka kwa wafanyabiashara hususani wanawake.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW