Mambo yatakayosaidia kumaliza tatizo la nishati Mkuranga

September 18, 2021 11:25 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Matumizi ya nishati jadidifu wakati wakisubiri umeme wa gridi ya taifa.
  • Wadau wa maendeleo wamesema wapo tayari kukopesha wafanyabiashara waliokidhi vigezo.
  • Watoa huduma za nishati wamesema zipo teknolojia za nishati jadidifu zinazoendana na hali ya kila mtu.

Dar es Salaam. Ndoto ya wafanyabiashara wengi kwenye Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ni kufikia kilele cha maendeleo na kuikomboa jamii inayowazunguka. 

Kwa wajasiriamali wilayani humo, ndoto kubwa ni kukuza biashara zao kwa kuongeza uzalishaji na kipato.

Ukosefu wa nishati ya umeme ya uhakika, inaweza kuwafanya watumie muda mrefu kuzifikia ndoto zao.

Mwenyekiti wa kikundi cha Juhudi Women Group kinachojishughulisha na utotoreshaji wa mayai wilayani humo, Oliva Lulandala ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, kukosekana kwa nishati ya umeme katika shughuli zake kunarudisha nyuma maendeleo ya kikundi hicho.

“Umeme unakatika kila siku kwa saa nne hadi 12. Endapo tukiwa na mayai kwenye mashine inasababisha tutumie jenereta liwashwe kwa saa nzima. Kwa siku umeme unapokatika usiku, inabidi tuwashe jenereta saa nane usiku,” amesema Lulandala.

Hali hiyo siyo tu inasababisha kelele za usiku kwa watu wanaozunguka banda lao la ufugaji bali matumizi ya petroli inayopanda takriban kila mwezi yanapunguza faida ambayo wangeipata endapo wangetumia umeme wa gridi ya Taifa.

Mbali na umeme kukatika, changamoto nyingine ni kuchelewa kufika kwa nishati katika vijiji vyote vya Mkuranga. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Afisa Maendeleo wa wilaya hiyo, hadi sasa, vijiji 87 kati ya 125 ndio vimefikiwa na umeme.

Hali hiyo inaviacha vijiji 38 gizani, jambo linalochangia matumizi makubwa ya kuni, mkaa na mafuta, nishati ambazo zinachangia katika uharibifu wa mazingira. 

Katika kutatua suluhu ya changamoto ya nishati katika wilaya hiyo, Mtandao wa Nishati na Jinsia Tanzania (Tangsen) uliandaa kongamano la kujadili masuala ya nishati wilayani humo lilofanyika Septemba 17, 2020 likikusanya wafanyabiashara, viongozi na wadau wa nishati.

Wakazi wa Mkuranga wanatumia kuni katika uzalishaji kwasababu ya ukosefu wa umeme. Picha| Thabit Mikidadi.

Matumizi ya majiko banifu

Kutokana na ukosefu wa wasambazaji wa nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia na umeme wamebaki wakitegemea kuni na mkaa.

Nishati hiyo ambayo siyo safi kwa ajili ya kupikia huwaacha baadhi wakiwa wagonjwa wa mfumo wa hewa na uoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Envotec, Sylvester Mwambiji amesema ni  wakati sasa kwa wananchi wa wilaya hiyo kuanza kutumia majiko banifu yanatotumia mkaa na kuni chache.

“Hatuwezi kukataa kuwa umeme hautoshi  na pia siyo wote wanaweza kumudu gharama za nishati jadidifu hasa kwenye uwekezaji. Kwa wananchi wa kawaida, yapo majiko yanayotumia kuni chache na hayatoi moshi wakati wa kupikia. 

“Pia yanahifadhi joto hivyo mtu hatotumia kuni nyingi na muda mwingi kupika,” amesema Mwambiji.

Mbali na hilo kwa wafugaji, wadau wa nishati wamependekeza matumizi ya mkaa mbadala kwenye ufugaji wa kuku kwa ambao hawajafikiwa na umeme. Endapo hilo litazingatiwa, ukataji wa miti utapungua.

Matumizi ya nishati jadidifu 

Mbali na Lulandala ambaye anapata hasara kwenye biashara yake ya kutotoresha mayai, wapo wengine ambao wana mashine za kusagia chakula cha mifugo ambazo hazifanyi kazi kwa sababu ya kutokufikiwa na umeme.

Mkurugenzi wa kampuni ya Ichi Renewable Energies inayojihusisha na masuala ya biogesi, Iqualiptus Malle amesema ipo mitambo ya biogesi ambayo ni ya gharama nafuu inayoweza kusaidia kufua umeme, kupika na kusaidia shughuli za uzalishaji.

Badala ya kunung’unika kutokana na changamoto za kukatika kwa umeme, Malle amewashauri wananchi hao kuangazia nishati mbadala ya kuwasaidia pale umeme unapookuwa umekatika.

“Mashine za kutotoreshea vifaranga, majiko ya kupikia yanaweza kuunganishwa na nishati ya biogesi. Pia yapo majenereta yanayoweza kufua umeme yanayoendeshwa na biogesi badala ya mafuta ya petroli,” amesema Malle.

Nishati nyingine ni pamoja na umemejua ambao ni rahisi kuupata. Umeme huo unaweza kutumika katika kuendesha mitambo na mashine za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo.

Hata hivyo, wadau wameshauri wananchi watengenezewe mfumo mzuri wa kupata nishati hizo ikiwemo kupatiwa mikopo na ruzuku. 

Afisa Masoko na Mauzo kutoka kampuni ya vifaa vya umwagiliaji vinavyotumia umemejua ya Simusola, Abdulrazak Nurdin amesema zipo kampuni ambazo zinatoa huduma ya mikopo ya vifaa vya kusaidia uzalishaji.

Simusola ni miongoni mwa kampuni hizo ambazo zinatoa mikopo ya pampu za maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ambazoo mtu anaweza kumaliza kulipa mkopo wake ndani ya miezi 22.

“Unapata mashine ya umwagiliaji ya Sh1 milioni na unalipa Sh250,000 kama bei ya kuanzia. Iliyobaki unalipa kidogo kidogo,” amesema Nurdin.

Pia, wanawake na vijana wametakiwa kuchangamkia mikopo ya halmashauri ili kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao ikiwemo nishati safi na salama ya mwanga, kupikia na uzalishaji.

Zipo nishati za kupikia, kuwasha taa na kufua umeme kwa ajili ya mitambo ikiwemo biogesi. Picha Ichi Energies.

Serikali yatoa msimamo

Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mkuranga, Peter Nambunga amesema ni heri kwa wananchi wa Mkuranga kuanza kutatua changamoto zao wenyewe na siyo kuisubiria serikali ifanye kila kitu kwani serikali inaendelea na shughuli za maendeleo kwa awamu.

Amesema badala ya kusubiri umeme uwafikie wale ambao haujawafikia, ni vyema wakaanza kutumia fursa zilizopo ikiwemo nishati jadidifu za umeme jua na biogesi.

“Hata vitabu vya dini vinatueleza kuwa, aliye nacho ataongezewa hivyo ndugu wana Mkuranga, tuanze na Serikali itakuja kuongeza pale tunapokwama,” amesema Nambunga.

Safari bado ndefu ya kuhakikisha kila wakazi wa Mkuranga wanapata nishati endelevu, safi na salama ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 98 ya wakazi wa wilaya hiyo  wanatumia kuni na mkaa kama nishati ya kupikia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW