Ukosefu wa ajira kwa walemavu wazidi kushuka Tanzania
- Ukosefu wa ajira miongoni mwa watu wenye ulemavu umeshuka hadi kufikia nusu ya kiwango kilichokuwepo miaka saba iliyopita.
- Ushiriki wao kwenye shughuli za uchumi unakua mdogo mdogo.
- Mikopo ya halmashauri yatajwa kuchochea kasi ya ukuaji katika ushiriki katika shughuli hizo.
Dar es Salaam. Baada ya kuwa nyuma katika fursa mbalimbali kutokana na mtazamo hasi wa jamii dhidi yao, idadi ya watu wenye ulemavu wanaojitosa katika shughuli za kiuchumi Tanzania imezidi kuongezeka kwa kasi ndani ya miaka saba iliyopita.
Ripoti ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi ya mwaka 2020/21 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya takwimu (NBS), inabainisha kuwa idadi ya watu wenye ulemavu wenye ajira imeongezeka hadi takriban theluthi mbili au asilimia 63.2 mwaka 2020/21 kutoka asilimia 59.1 mwaka 2014.
Hiyo inamaanisha hadi mwaka jana takriban watu sita kati ya 10 wenye ulemavu walikuwa na ajira ama kwa kujiajiri au kuajiariwa.
Katika kipindi hicho, kiwango cha watu wenye ulemavu wenye umri miaka 15 na zaidi ambao hawakuwa na ajira nacho kilishuka.
Ushiriki wa watu wenye ulemavu katika shughuli mbali mbali za uzalishaji unachangia katika ukuaji wa uchumi nchini. Picha| ITV.
Takwimu hizo zinaeleza zaidi kiwango cha watu wenye ulemavu mwaka 2020/21 kilikuwa asilimia 6, nusu ya kile kilichokuwepo mwaka 2014 ambacho kilikuwa asilimia 12.4.
“Kuanzishwa kwa dirisha maalumu la mikopo kwa watu wenye ulemavu (asilimia 2 ya mapato ya ndani ya halmashauri) kumechangia ukuzaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya NBS.
Ili kuwepo na uendelevu wa hali nzuri, ripoti hiyo inaeleza kuwa zinahitajika juhudi kubwa katika kuingiza masuala ya walemavu kwenye sera nyingine ili wasiachwe nyuma.
Soma zaidi
- Teknolojia ya umeme tayari kuwanufaisha walemavu, wazee
- Vijana, wanawake walemavu wanavyowezeshwa kujitegemea kiuchumi
- Huyu ndiye shujaa wa watu wenye ulemavu Tanzania
Kwa muda mrefu nchini Tanzania kumekuwa na dhana kuwa mlemavu ni mtu anayepaswa kuwa tegemezi katika jamii jambo ambalo si kweli.
Baadhi ya watu huenda mbali zaidi na kuwaficha watu wenye ulemavu ili wasionekane na jamii kiasi cha kuwakosesha fursa za kijamii na kiuchumi ikiwemo elimu na mitaji.
“Hatua hizi ni lazima ziendane na zoezi la kuwabainisha na kuwasijili watu wenye ulemavu katika jamii,” ripoti hiyo iliyozinduliwa Novemba 2021 inaeleza.
