Serikali kuwatafutia Watanzania ajira katika nchi nane
- Mpaka sasa kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu kuna ajira 67,475 za Watanzania nje ya nchi.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inatarajia kuingia makubaliano na nchi nane duniani zikiwemo za Umoja wa Falme za Kiarabu ili kuwawezesha Watanzania wenye ujuzi kufanya kazi nje ya nchi ikiwa ni miongoni mwa jitihada za kupanua wigo wa ajira.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi amelieleza Bunge leo, Novemba 6, 2024, jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu, kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa jitihada za kuwatafutia ajira Watanzania baada ya Tanzania kuingia makubaliano na nchi tatu.
Katambi alikuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum Ester Maleko kuhusu hatua za Serikali kuhakikisha Watanzania wanapata ajira nje ya nchi.
Ukosefu wa ajira hususan kwa vijana ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayoikabili Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, jambo linalochochea kuongezeka kwa utegemezi miongoni mwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2020/21 wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) takriban watu 10 kati ya watu 100 au asilimia 9 ya watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi hana ajira.
Dar es Salaam ndiyo mkoa unaongoza Tanzania Bara kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira. Watu wawili kati ya 100 jijini Dar es Salaam, hawana ajira ikiwa ni mara mbili ya wastani wa kitaifa.
“Makusudio yetu ni kuhakikisha tunaingia kwenye makubaliano na nchi nane zikiwemo nchi za umoja wa nchi za Kiarabu ili kuhakikisha Watanzania wanafanya kazi huko na wameshakwenda kwa awamu mbalimbali,” amesema Katambi bila kutaja nchi nyingine.
Novemba 2023 Serikali ilisaini mikataba miwili na serikali ya Saudi Arabia kwa ajili ya kuweka mifumo ya ajira kwa ajili ya Watanzania na mifumo ya kudhibiti mchakato wa kuajiri wafanyakazi wa kitaalam na majumbani.
Serikali, amesema, inawatumia mabalozi waliopo nje ya nchi kutafuta fursa za ajira kwa Watanzania ambao hufuatilia na kuwasiliana na Wizara ya Kazi pindi fursa zinapotangazwa wakati huo wakishirikiana na Diaspora.
Ili kupata kazi hizo, amesema juhudi binafsi za Watanzania wenye ndoto za kufanya kazi nje ya nchi, visomo, sifa na vigezo ni miongoni mwa vigezo vitakavyo wawezesha kufanya kazi katika nchi zenye fursa ya ajira.
Kwa mujibu wa Katambi amesema katika kuhakisha Serikali inafikia adhma ya ajira kutoa ajira milioni nane ifikapo mwaka imeweka mpango wa kuhakikisha kila mwaka inaweka ajira 1.2 milioni na kwa mwaka 2024 kuanzia Januari – Julai ni kuna ajira 67,475 za Watanzania nje ya nchi.
Katambi amesema kuna utafiti unaendelea kufanywa kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Waziri Mkuu, na Benki ya Dunia, kupitia ‘Integrated Labour Force Survey’ ili kupata takwimu sahihi za ajira zinazohitajika pamoja na mapato ya ajira.