Uhaba wa maji unavyowatesa wananchi Mwanza

June 27, 2020 11:57 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wakazi wa kijiji cha Identemya Wilaya ya Usagara mkoani humo wanaoutumia maji ya madimbwi.
  • Wanalazimika kutembea kilomita 10 kufuata maji safi. 
  • Serikali yasema inatekeleza miradi ya maji itakayokifikia kijiji hicho. 

Mwanza. Licha ya wakazi wa kijiji cha Identemya Wilaya ya Usagara mkoani Mwanza kuishi karibu na Ziwa Victoria bado wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama ya bomba. 

Hali hiyo imewalazimisha kutumia maji ya madimbwi na wakati mwingine hutembea umbali wa kilomita 10 kufuata maji katika vijiji vya jirani. 

Wakazi hao wanaoishi takriban kilomita 20 nje ya jiji la Mwanza, Ili wayapate maji hayo hutumia Sh500 hadi Sh1,000 kununua ndoo ya maji ya lita 20. 

Balozi wa kijiji cha Identemya Juma Masasi amesema kutokana tatizo la uhaba wa maji wanalazimika kutumia maji ya madimbwi ambayo yanavimelea vya wadudu wanaosababisha magonjwa ya tumbo, kichocho na kuharisha.

“Tunaomba Serikali itusaidie upatikanaji wa maji safi, kwani tunahagaika sana hususan kipindi hiki cha kiangazi ambapo hata madimbwi tunayotumia kuchota nayo yanakauka,”amesema Masasi.

Balozi wa kijiji cha Identemya, Juma Masasi mwenye shati jeupe akichota maji kwenye dimbwi. Picha| Mariam John.

Wakazi hao wamepaza sauti zao, siku chache baada ya Mamlaka ya Maji Safi na Ssafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa) kubainisha kuwa imeongeza wateja wa maji safi kutoka 21,824 mwaka 2016 hadi 80,953 mwaka jana.

Prisca Ngusa ni mmoja wa wakazi wa kijiji hicho anasema hulazimika kuamka alfajiri na mapema kufuata maji ya kunywa kwenye madimbwi lakini anapofika eneo hilo hukutana na foleni ndefu ya watu.

“Maji tunayotumia yananuka tope kwa kuwa tunachangia na wanyama lakini pia watu wengine huyatumia kwa matumizi yao binafsi kama kufyatulia tofari hata shughul za ujenzi,” amesema Prisca.

Ameiomba Serikali ya Tanzania kuwapelekea mabomba ya maji kama wanavyofanya sehemu nyingine kwa kuwa wanaishi karibu na Ziwa Victoria.

Hata hivyo, Serikali imesema inaendelea kutekeleza miradi ya maji kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuhakikisha kila kijiji nchini kitapata huduma ya maji safi na salama. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwauwasa, Leonard Mseng’ele  amesema ofisi hiyo bado inatekeleza miradi mbalimbali ya maji ikiwemo ujenzi wa kituo kikubwa cha kusambazia maji katika eneo la Butimba ambacho kitapeleka maji katika eneo la Buhongwa, Kisesa, Nyamhong’olo na Kishiri.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo itachangia katika kuongeza makusanyo ya maji  kutoka Sh2 milioni kwa mwezi hadi Sh2.4 milioni kwa mwezi lakini pia itaongeza wateja wengine wapya.

Amesema kwa sasa mpamgo uliopo ni kupeleka maji katika meneo ya mwinuko na yaliyoko nje ya jiji.

Huenda mipango hiyo Mwauwasa ya kupeleka maji nje ya jiji ikiwanufaisha wanakijiji wa Identemya bado hawajafikiwa na huduma ya mabomba ya maji. 


Soma zaidi:  Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano utunzaji bonde la mto Nile


Katibu Mkuu wa Wizara ya maji, Profesa Kitila Mkumbo akiwa jijini Mwanza hivi karibuni alitoa changamoto kwa mamlaka hiyo kuhakikisha inamaliza tatizo la upatikanaji wa maji maeneo ya mjini.

Amesema ni aibu kwa jiji kama Mwanza ambalo lina chanzo cha maji kutoka Ziwa Victoria kushindwa kulitumia katika kuwapatia huduma hiyo wakazi wake na badala yake watu wanaokaa nje ya Mwanza wanapata huduma hiyo kirahisi.

“Haiwezekani mkazi anayeishi mbali na ziwa kama Shinyanga, Tabora anapata huduma ya maji kutoka kwenye chanzo kikuu wakati wakazi wanaoishi mita chache na chanzo hicho walilie maji hii sio jambo zuri ni vema likafanyiwa kazi haraka iwezekano,” amesema Professa Mkumbo.

Pia ameitaka mamlaka hiyo kumaliza tatizo la ukatikaji wa maji na kuelekeza Wahandisi kulitafutia suluhu suala hilo. 

“Siyo kila umeme ukikatika na maji yanakatika na mnatoa taarifa kwa wakazi wenu kuchukua tahadhari, wakati mwingine muwafanye wateja wenu wasijue kama kuna tatizo la upatikanaji maji lazima mjenge kituo cha kudumu cha kusambaza maji,” amesema Mkumbo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW