Chanzo kipya kutibu uhaba wa maji wilayani Ilemela
- Kitajengwa katika Mtaa wa Kabagaja uliopo wilayani humo.
- Kinategemewa kuzalisha lita milioni 20 za maji kwa siku.
Mwanza. Huenda wakazi wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wakaondokana na kero ya uhaba wa maji wilayani humo mara baada ya Serikali kubainisha kuwa imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa chanzo kipya cha maji ili kuongeza uzalishaji jambo litakalosaidia kupunguza uhaba wa huduma hiyo muhimu.
Wilaya ya Ilemela inakabiliwa na upungufu wa lita milioni 20 za maji kila siku kutokana na vyanzo vyake kutokidhi mahitaji ya lita milioni 160 zinazotakiwa.
Chanzo hicho kipya ambacho kitaanza kujengwa mwaka huu wa fedha wa 2023/24 katika Mtaa wa Kabagaja wilayani humo kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 20 za maji kwa siku na hivyo kufidia upungufu uliopo.
Kwa sasa Ilemela inategemea chanzo cha maji kilichopo Butimba kinachozalisha lita 148 huku kikihudumia manispaa ya jiji pamoja na wilaya hiyo jambo linalosababisha uhaba wa maji.
Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wakazi wa Ilemela amewaambia kuwa mbali na kujenga chanzo hicho Serikali itafufua visima vinne vya maji ili kutatua changamoto iliyopo.
“Nikiri kwamba ni kweli Ilemela inakabiliwa na changamoto ya maji na hii ni kutokana na ongezeko la watu na pili ni miundombinu ya kusambaza maji ambapo wakati inatengenezwa ilikuwa na uwezo wa kusambazia maji kwa watu laki tano kwa jiji nzima la Mwanza, lakini sasa sensa ya mwaka jana ilemela ilikuwa na watu milioni 3,” amesema Mabula
Mabula ameongeza kuwa pamoja na kujengwa chanzo hicho kipya cha Kabagaja idara ya maji jijini humo inapaswa kubadilisha miundombinu na kuweka yenye uwezo wa kuhudumia wananchi kwa uharaka.
Kutokana na malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusiana na mgao wa maji wa mara kwa mara pamoja na kutozwa bili kubwa injinia wa maji kanda ya Sabasaba, Melichades Eustao amesema wanalazimika kutoa mgao wa maji kutokana na miundombinu kushindwa kusambaza maji kwenye maeneo yote kwa kuwa jiografia ya eneo hilo lina milima mingi.
Latest