Ugonjwa wa Uviko-19 hauwapati matajiri pekee

August 22, 2022 6:22 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kila mtu yupo kwenye hatari ya kupata Uviko-19.
  • Chanjo ya Uviko-19 pekee ndiyo inaweza kupunguza hatari ya vifo na maambukizi.

Dar es Salaam. Kumekuwa na habari zinasombaa mtandaoni kuwa watu wenye kipato cha chini hawapati virusi vya Uviko-19 jambo ambalo si kweli. 

Mfano, mmoja wa watumiaji wa Facebook aliandika kuwa Uviko-19 unawapata “walamba sukari” na “kuwaogopa” wenye “maisha magumu”. 

Walamba sukari kwa muktadha wake akimaanisha kuwa watu matajiri pekee ndiyo hukumbwa na maradhi, kauli ambayo ni uzushi na haijathibitishwa kitaalamu.


Hakuna ukweli wowote kwamba ugonjwa wa Uviko-19 unawashambulia watu wenye kipato cha juu na kuwaacha wenye kipato cha chini kama Rebeka J Pimbili alivyotoa maoni kwenye ukurasa wa Facebook.

Mchangiaji huyo alitoa maoni kwenye ukurasa wa chombo cha habari cha ITV uliokuwa umechapisha habari kuhusu kuhamasisha chanjo ya Uviko-19, Julai 25, 2022.


Soma zaidi:


Tunachokifahamu

Wataalamu mbalimbali wa afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) wanaonya kwamba kila mtu yupo kwenye hatari ya kupata virusi hivi bila kujali rangi yake, hali ya kifedha, umri au eneo analoishi. 

Shirika la  Fedha la Kimataifa  (IMF) nalo linasema vijiji masikini ulimwenguni kote vimepata maambukizo na vifo vingi vya Uviko -19 kuliko tajiri na kusababisha athari zaidi kwa watu wenye kipato cha chini katika nchi zote.

Moja ya watu mashuhuri na wenye uwezo waliothibitisha hadharani kupata Uviko-19 ni msanii wa bongo fleva Hamisi Mwinjuma maarufu kama MwanaFa ambaye  Machi 19, 2020 kupitia ukurasa wake wa Instagram  aliweka wazi kuambukizwa virusi hivyo.

Si watu wa bara la Afrika tu wanaopitia misukosuko ya gonjwa hili.  Hivi karibuni Ikulu ya Marekani ilieleza kuwa Rais wa taifa hilo Joe Biden aliambukizwa virusi vya Uviko-19 Julai 22 mwaka huu na baada ya siku tano za kujitenga alipona. 

Uamuzi wetu

Kutokana na  ushahidi huo, ni wazi kuwa kipato au hali ya uchumi haimzuii mtu yoyote kupata maambukizi ya virusi vya Uviko-19. Madai kuwa maradhi hayo yanawapata matajiri ni uzushi unaolenga kuongeza hatari ya watu kupata Uviko-19 nchini. 

Hadi sasa chanjo ya Uviko-19 ndiyo njia pekee inayoweza kupunguza hatari zaidi ya kifo dhidi ya maradhi hayo. 

Serikali inaendelea kusisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huu hususan kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko na kuchanja ili kuhakikisha usalama wao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW