Mambo ya kuzingatia katika uchaguzi, maandalizi ya chakula bora

August 19, 2024 6:34 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Usafi ni jambo la kuzingatia katika maandalizi ya chakula.
  • Ni muhimu kwa mtumiaji kujua uimara wa bidhaa. 

Dar es salaam. Usalama wa chakula ni miongoni mwa masuala muhimu ya kuzingatia kabla na baada ya maandalizi ya chakula ili kulinda afya za walaji. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) takribani watu milioni au mmoja kati ya 10 hupata maradhi kutokana na ulaji wa chakula kisicho salama na kusababisha vifo 420,000 kila mwaka.

Ili kupunguza idadi ya vifo na magonjwa yatokanayo na tatizo hilo Jukwaa la Ubora Tanzania (NQAT) limetoa elimu kwa wananchi juu ya uzingatiaji wa viwango vya usalama wa chakula ili kuhakikisha upatikanaji wa lishe bora kwa wote.

Dk Ester Nkuba mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) aliyekuwa akizungumza katika jukwaa hilo lililofanyika Agosti 17,2024 jijini Dar es Salaam amesema miongoni mwa mambo ya kuzingatia katika maandalizi ya chakula ni usafi.

“Ili chakula kiwe safi na salama kwa mlaji ni muhimu kuangalia usafi wa mazingira ya kuandaa chakula, wewe mwenyewe ni msafi, umenawa mikono na hata kama umenawa unaweza kuacha vijidudu kwenye mikono yako,” ameongeza Dk Nkuba.

Zingatia namna bora ya kuandaa mboga ya majani

Mbali na kuzingatia suala zima la usafi Dk Nkuba anabainisha kuwa ni vyema kuzingatia namna bora za uandaaji wa mboga za majani ili kutunza virutubisho vyenye umuhimu katika mwili wa binadamu.

Amesema kuwa mboga za majani ni lazima zioshwe kisha zikatwe kwa namba inayohitajika kitaalamu ili kumnufaisha mlaji.

“Kitalaamu tunashauri kwamba mboga za majani zioshwe ndio zikatwe katwe na zinapo katwa katwa zikatwe vipande vikubwa ili kutopoteza virutubishi vilivyomo katika zile mboga…

…Yale maji ya kijani yanayoonekana wakati wa kuosha mboga yanaenda pamoja na virutubishi vya vitamini A na vitamini B na sio hivyo tu mboga zinazopikwa ziwekwe mafuta ili kufyoza virutubishi kwenye mwili,” amesema Dk Nkuba.

Hata hivyo, Dk Nkuba ameongeza kuwa katika utunzaji wa vyombo vya kutumia ni vyema mtu kuanika vyombo kwenye kichanja kuliko kutumia vitambaa kufuta vyombo ambavyo kwa njia moja au nyingine huweza kutunza wadudu.

Zingatia ubora wa bidhaa 

Mhandisi Deus Maganga aliyekuwa mmoja kati ya wazungumzaji katika jukwaa hilo amesema kuwa uzingatiaji wa ubora wa bidhaa una mchango mkubwa katika kuboresha afya na maisha kwa ujumla.

Maganga ameongeza kuwa mtumiaji anapaswa kujua uimara wa bidhaa hususani za chakula ikiwemo uwezo wa bidhaa kudumu kwa muda mrefu bila kuharibika kabla ya kuanza kutumia.

Chakula bora na salama ni kipi?

Joyline Ndanshau mtaalamu wa Sayansi na Teknolojia ya Chakula kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amebainisha kuwa chakula salama na  bora ni chakula ambacho hakina vihatarishi ambavyo vinaweza kuleta madhara kwa mlaji.

“Kwa mfano unakula wali unakutana na mchanga ni kihatarishi au unakula nyama unakutana na kipande cha mbao,” amesema Ndanshau.

Aidha, Ndanshau ameongeza kuwa watu wanapoandaa chakula wanapaswa waandae kwa usalama huku wakiwa wanaelewa kuwa kuna madhara yanayotokana na chakula.

“Kuna wakati unakula chakula tu tumbo linakuuma au unaenda hospitali unaambiwa ni ‘food poisoning’ sio kwamba umewekewa sumu hapana ni namna ambayo chakula hakikuandaliwa kiusafi,”ameongeza Ndanshau.

Naye Safari Fungo, miongoni mwa waanzilishi wa Jukwaa la Ubora Tanzania amebainisha kuwa lengo la jukwaa hilo nikuwaleta pamoja wadau wa sekta mbalimbali ili kuangalia mambo ya ubora wa chakula na usalama katika maeneo ya uzalishaji na huduma ili kuongeza uelewa kwa wananchi. 

Enable Notifications OK No thanks