UDSM, SUA, Mzumbe vyadakwa na nyavu za CAG

April 10, 2020 8:46 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • CAG aeleza kuwa vyuo hivyo na vingine vilishindwa kufuatilia ufanisi wa wahitimu wake waliopo kazini licha ya kuwa na bajeti zake 
  • Kichere asema hali hiyo husababisha vyuo kushindwa kufanya maamuzi sahihi ya kuboresha elimu inayotolewa.

Dar es Salaam. Unaweza kusema vyuo vikuu vikubwa Tanzania vimeingia kwenye nyavu za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere baada ya ripoti ya CAG kubaini kuwa baadhi ya taasisi hizo zimeshindwa kufuatilia ufanisi wa elimu waliyoitoa kwa wahitimu wake waliopo kazini. 

Ripoti ya CAG kuhusu Mashirika ya Umma ya mwaka 2018/2019 imezitaja taasisi hizo za elimu ya juu nchini kuwa ni Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Kichere amesema moja ya malengo katika mpango-mkakati wa Chuo Kikuu cha Mzumbe wa 2017/2018 – 2021/2022 ilikuwa ni kufuatilia ufanisi wa wanafunzi waliohitimu mafunzo katika chuo (Tracer Study) hicho ili kufahamu iwapo elimu iliyotolewa ilikuwa na manufaa kwa wanafunzi kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi. 

Zoezi hilo la ufuatiliaji lilipangwa lifanyike kwa kila kitivo, shule kuu au taasisi ya Mzumbe ifikapo mwezi Juni 2022 lakini kilifanya zoezi moja tu la kufuatilia ufanisi wa wanafunzi waliohitimu.  

 Akizungumzia Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, ripoti hiyo imeeleza kuwa huo hicho kilipanga kutekeleza mazoezi sita ya ufuatiliaji wa ufanisi wa wanafunzi waliohitimu kati ya kozi 29 zinazotolewa na chuo katika mpango-mkakati wake wa mwaka 2016/2017-2020/2021 lakini hakikufanya kikamilifu. 

“Nilipohitaji kupewa taarifa kamili ya zoezi la ufuatiliaji wa ufanisi wa wanafunzi, sikupewa kwa sababu zoezi la mwisho la ufuatiliaji wa wanafunzi lilifanyika mwaka 2004,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 

Hata hivyo, CAG amebaini kuwa chuo hicho kilifanya zoezi moja la ufuatiliaji wa wanafunzi katika kozi moja tu kati ya kozi 29, ambapo Chuo kilitumia Sh97.45 milioni kati ya bajeti ya Sh480 milioni iliyopangwa kutumika kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2016/2017 hadi mwaka 2018/2019. 


Soma zaidi:


Pia, CAG amebaini kuwa Chuo cha OUT, UDSM na NIT havikufanya zoezi la ufuatiliaji wa ufanisi wa wanafunzi baada ya kuhitimu. 

Amesema Mpango-mkakati unaonyesha kuwa OUT kilijiandaa kuwa na mkakati wa ufuatiliaji wa ufanisi wa wanafunzi kufikia mwezi Juni 2020, lakini miezi sita kabla ya kufika muda uliopangwa, chuo hakikuwa kimepanga na kutekeleza shughuli zozote kufikia lengo hilo. 

UDSM nacho kimebainika kuwa hakikutenga bajeti kwa ajili ya kufanya zoezi hilo na mara ya mwisho kufanyika zoezi la ufuatiliaji ilikuwa mwaka 2003. “Hali hii inatengeneza ombwe la muda wa miaka 16 toka zoezi lilipofanyika,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.  

Hata hivyo, NIT kiliweza kufuatilia baadhi ya wanafunzi kupitia mfumo wa “Alumina Portal” ambapo kwa sasa, Chuo kinatekeleza mradi wa Benki ya Dunia ambao moja ya kazi zinazofanyika ni kufuatilia ufanisi wa wanafunzi waliohitimu. 

Kwa kupitia mradi huo, wafanyakazi wanne wamepewa mafunzo ya jinsi ya kutekeleza zoezi la ufuatiliaji wa ufanisi wa wanafunzi ambalo limepangwa kutekelezwa katika mwaka 2019/2020.

Ukumbi wa Nkurumah uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao hutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo mihadhara ya wasomi. Picha|Mtandao.

Athari za kutokufuatilia ufanisi wa wahitimu

Ripoti ya CAG imesema kutokana na kutofanyika kwa zoezi hili la ufuatiliaji wa ufanisi wa wanafunzi, vyuo hivyo vinashindwa kuhusianisha elimu wanayoitoa na mahitaji ya soko la taaluma.

“Hivyo, vyuo vinashindwa kufanya maamuzi sahihi ya kuboresha elimu inayotolewa. Zaidi ya hilo, utungaji wa mitaala ya kufundishia inaweza isihusishe mrejesho wa soko juu ya taaluma ili kujua maeneo ya kufanyia mabadiliko,” imeeleza ripoti hiyo. 

Uongozi wa vyuo husika umeshauriwa kutengeneza mfumo wa kufanya zoezi la ufuatiliaji wa ufanisi wa wanafunzi na kuhakikisha maboresho ya mtaala ya kufundishia yanajumuisha mrejesho wa taarifa ya ufuatiliaji wa ufanisi wa wanafunzi waliohitimu ili kukidhi mahitaji ya soko la taaluma.

Enable Notifications OK No thanks