Udom kusitisha udahili kozi tisa za ualimu, wadau wa elimu watoa neno
- Wadau washauri wanafunzi kuangalia vyuo vingine vinavyotoa kozi hizo zilizositishwa.
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimesitisha udahili wa wanafunzi katika programu tisa za shahada ya kwanza za ualimu kwa mwaka wa masomo 2025/2026 ikiwemo ualimu wa Sayansi, Saikolojia, Biashara, Sanaa, Mafunzo ya Habari na Mawasiliano, pamoja na Elimu ya Watu Wazima.
Hii ina maana ya kwamba kwa wale waliokuwa na ndoto za kusoma kozi hizo kupitia chuo cha Udom wanapswa kutafakari upya matamanio yao na kuangalia njia mbadala.
Taarifa hiyo imetolewa rasmi siku ya Ijumaa Julai 18, 2025 na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu kupitia tovuti ya chuo hicho.
Mpaka sasa chuo cha Udom bado hakijaweka wazi sababu za kufikia maamuzi hayo, Nukta TV ilifanya jitihada za kupata ufafanuzi wa jambo hilo ambapo Afisa habari wa chuo hicho Rose mdami ameeleza kuwa taarifa rasmi ya chuo itatoka baada ya wao kupokea majibu ya barua waliyoiandika kwenda Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen lililofanya mahojiano na Makamu Mkuu wa Chuo cha Udom, Profesa Lughano Kusiluka, chuo hiko kiko kwenye majadiliano na wadau wote muhimu akiwemo mdhibiti (TCU) na kitaweka wazi taarifa kamili baada ya mchakato kukamilika.
Hata hivyo, wadau wa elimu wamekuwa na mitizamo tofauti kuhusiana na suala hilo,Injinia Aviti Mushi, mwandishi wa vitabu na Mhadhiri wa Uhandisi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) amesema licha ya kuwa chuo hicho hakijataja sababu ya uamuzi huo anadhani huenda umechangiwa na ukosefu wa soko la uhakika wa ajira kwa wahitimu wake au chuo kutokuwa na uwezo wa kufundisha wanafunzi katika kozi husika.
“Labda wamezibadilisha kwa sababu wameona watawafundisha watu na watu watatoka lakini katika soko la ajira watapata shida, watashindwa kujiajiri au hawataweza kuajiriwa,” ameeleza Injinia Mushi.
Aidha, Injinia Mushi amesema uamuzi huo ukiridhiwa na TCU utakuwa na athari hasi na chanya katika sekta ya elimu nchini.
Akielezea athari hasi Mushi amesema licha ya kuwa chuo kitakosa mapato ambayo yangepatikana kwa wanafunzi kulipa gharama za ada na udahili jamii itakosa wataalamu ambao wangezalishwa kwa kusoma kozi hizo na hivyo kutakuwa na upungufu.
“Kama wameondoa kozi tisa tuseme kila kozi ilikuwa inachukua wanafunzi 20 ina maana ni wanafunzi 180 hao, je wanafunzi 180 wanaweza kusoma kozi nyingine? Nafasi zipo? Kama inawezekana ni vizuri wataenda kusoma hizo kozi nyingine kama haiwezekani hiyo ni changamoto kwao watakuwa wamekosa hiyo fursa,” amefafanua Injinia Mushi.
Licha ya uwiano wa walimu na wanafunzi kuimarika kwa siku za hivi karibuni bado haujafikia viwango vilivyowekwa na Serikali ambavyo ni kuwa na mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.
Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi cha mwaka 2023, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika shule za Serikali ulikuwa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 61 ikilinganishwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 63 mwaka 2022.

Richard Mabala mwandishi wa vitabu na Mdau wa elimu nchini Tanzania ameiambia nukta TV kwamba licha ya chuo hicho kutoweka wazi sababu za kusitisha udahili wa kozi hizo, bado uhitaji wake upo kwa kuwa Tanzania bado inakabiliwa na utoshelevu wa walimu katika ngazi mbalimbali za elimu.
“Kwa hali ya kawaida tunahitaji walimu wengi zaidi, lakini walimu wengi wanakanyaga rami, licha ya walimu ambao hawaajiriwi lakini kuna uhaba sana wa walimu katika shule. Kwa ujumla upande wa walimu hawatoshi hivyo kutotosha kwa walimu kunaleta mgawanyiko wa kitabaka,” amesema Mabala.
Hata hivyo, Mabala ameeleza kuwa iwapo Udom wamesitisha udahili wa fani hiyo, wanafunzi wenye uhitaji wa kusoma bado wanayo nafasi ya kusoma katika vyuo vingine.
“Kuna nafasi nyingi za kusoma kama Udom hawatoi basi waende kwenye chuo kingine,” ameeleza Mabala huku akiwataka wanafunzi kuangalia vyuo vingine.
Latest
