JAB yawafungia watangazaji wanne MJini FM kwa kukiuka maadili
- Yasema kipindi chao kilikuwa na maudhui yaliyojaa uchambuzi usio wa kitaaluma, ukiukaji wa maadili ya habari na uvunjifu wa sheria.
Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewafungia watangazaji wanne wa kituo cha redio cha Mjini FM baada ya kubainika kukiuka maadili ya taaluma ya habari na Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023).
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa JAB Patrick Kipangula, leo Julai 18, 2025 imeeleza kuwa watangazaji waliofungiwa ni Deodatha William, Mussa Crispin Mgenge, Perfect Crispin na Iddy Bakari Iddy waliomhoji msanii wa muziki wa Singeli anayejulikana kama Dogo Paten.
Kipangula amesema uamuzi huo umetolewa baada ya uchambuzi wa kitaalamu wa mahojiano yaliyofanyika Julai 16, 2025, katika kipindi cha mubashara cha genge la Gen Tok ambapo walibaini kipindi hicho kilikuwa na maudhui yaliyojaa uchambuzi usio wa kitaaluma, ukiukaji wa maadili ya habari na uvunjifu wa sheria.
“Watangazaji hao walikiuka haki ya faragha na kutweza utu wa mhojiwa kwa kumlazimisha kutoa taarifa binafsi bila ridhaa yake kinyume na Kanuni ya 11(1)(e) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji ya Redio na Televisheni), 2018 (kama zilivyofanyiwa marekebisho),” amesem Kipangula kwenye taarifa yake.
Aidha, Kipangula amesema Watangazaji hao walitumia lugha ya kumshushia hadhi mhojiwa kinyume na Kanuni ya 11(1)(f) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji ya Redio na Televisheni), 2018 (kama zilivyofanyiwa marekebisho) na Kanuni ya 16(1), ikisomwa pamoja na Jedwali la Tatu aya ya 2(b) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2020.
Wakati huo huo, JAB imebaini watangazaji hao, watangazaji hao hawajasajiliwa na kupewa ithibati na bodi hiyo, hivyo wanafanya kazi za kihabari kinyume na Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023).
Kutokana na makosa hayo JAB imewapiga marufuku watangazaji hao kujihusisha na masuala ya kihabari kuanzia leo Julai 18, mpaka hapo watakapotimiza matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na sifa za kielimu na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.
Kipangula, amesema hatua hiyo ni onyo kwa vyombo vyote vya habari vinavyopuuza misingi ya taaluma ya habari, kwa kuwa ni mhimili wa utawala bora, hivyo unapaswa kuendeshwa kwa weledi, uadilifu na heshima kwa utu wa binadamu.
Aidha, amewakumbushwa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanaofanya kazi za uana habari kwenye vyombo vyao wamesajiliwa na kupewa ithibati na bodi ya ithibati ya waandishi wa habari.
Latest



