Uchunguzi chanzo ajali ya ndege Ziwa Victoria waanza

November 7, 2022 12:08 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link


  • Serikali yasema timu ya wataalam imeshaanza uchunguzi.
  • Wavuvi walioshiriki uokoaji kupigwa msasa zaidi kwa mafunzo ya uokozi.
  • Wakuu wa mikoa kusimamia mazishi ya wahanga.

Dar es Salaam. Wakati miili ya watu 19 waliopoteza maisha katika ajali ya ndege Ziwa Victoria ikiaagwa leo, Serikali imesema inaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo huku ikiagiza wavuvi katika ziwa hilo kupewa mafunzo ya uokozi. 

Serikali imesema inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali ya ndege ya abiria ya Shirika la ndege la Precision Air iliyotokea jana Novemba 6,2022 majira ya asubuhi wakati ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Kaitaba mkoani Kagera.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaambia wananchi waliojitokeza kuaga miili ya watu waliopoteza maisha katika uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba kuwa timu ya wataalamu kwa ajili ya uchunguzi imeshaanza kazi hivyo wananchi wawe watulivu.

“Kwa sasa timu ya wataalamu inaendelea kufanya uchunguzi wa awali kubaini chanzo cha ajali. Niwasihi wananchi utulivu mpaka hapo timu ya wataalamu itakapokamilisha na kutoa taarifa ya uchunguzi,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana


Waziri Mkuu amesema wavuvi walioshiriki katika zoezi la kuokoa manusura wa ajali watapewa mafunzo ya ziada kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili wajiimarishe katika kukabiliana na dharula kama hizo pale zinapotokea.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Precision Air Patrick Mwanri ndege hiyo yenye namba PW 494 ilikuwa imetokea jijini Dar es Salaam ikiwa na watu 43 wakiwemo abiria 39, wahudumu wawili na marubani wawili.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza Serikali kugharamia mazishi ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ambayo yatasimamiwa na wakuu wa mikoa pamoja na kamati za usimamizi wa maafa za mikoa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanahisiwa kuwa ndio chanzo cha ajali hiyo yalianza kutokea majira ya saa mbili na dakika 20 asubuhi wakati rubani akiwa katika hatua za mwisho za kutua.

“Wakati hali ya hewa inabadilika kulikuwa na mvua zilizoambatana na radi, upepo mkali na mgandamizo wa kwenda chini (down gravity),” amesema Prof Mbarawa.

Mbarawa amesema wataeleza kwa kina chanzo cha ajali hiyo uchunguzi utakapokamilika na kwa sasa wanaendelea kufanya jitihada za kuiondoa ndege iliyopata ajali uwanjani ili shughuli za usafiri zilizoathiriwa na ajali hiyo ziendelee kama kawaida ambapo kwa sasa ni ndege ndogo tu ndio zina uwezo wa kutua.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...