Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 6 ifikapo 2025
- Ukuaji huo utachangia kuongezeka kwa uwekezaji na ukuaji wa sekta mbalimbali nchini.
Arusha. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limetabiri kukua kwa uchumi wa Tanzania kwa asilimia 6 mwaka 2025 kutoka asilimia 5.1 iliyorekodiwa katika mwaka huu wa fedha.
Ripoti ya hali ya uchumi wa dunia iliyotolewa na IMF Oktoba, 2024 imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 barani Afrika ambazo uchumi wake unatarajiwa kukua kwa kasi kwa mwaka ujao.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Oktoba 24, 2024 amesema makisio hayo yatachangia kuongezeka kwa uwekezaji na ukuaji wa sekta mbalimbali nchini.
“Hii ni habari njema kwetu na tungependa Watanzania waifahamu. Kutokana na ukuaji huu wa uchumi, tunatarajia kupokea ongezeko kubwa la uwekezaji, kukua kwa sekta nyingine kama Kilimo, Viwanda, Utalii, na sekta zinginezo…
…Hali itakayochangia kupunguza umasikini kwa mtu mmoja mmoja na kuboresha hali ya maisha ya kila siku,” amesema Makoba.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya IMF inatofautiana na Wizara ya Fedha ambayo ilikadiria kukua kwa uchumi wa Tanzania kwa asilimia 5.4 kwa mwaka 2024/25 ukiongezeka kwa asilimia 0.3 kutoka ule uliorekodiwa mwaka uliopita,
Tanzania imerekodi kupanda na kushuka kwa uchumi tangu kutokea kwa janga la janga la Uviko 19 mwaka 2019 na 2020.
Mwaka 2021 Tanzania ilirekodi ukuaji wa uchumi wa asilimia 4.8 iliyoshuka hadi asilimia 4.7 mwaka 2022 na baadae kuongezeka hadi asilimia 5.1 mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ukuaji huo wa uchumi umechangia kuvutia uwekezaji ambapo katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2024 miradi mikubwa 1,350 yenye thamani ya Dola za Marekani 12.2 bilioni.
“Kati ya mirafdi hiyo 866 inahusissha wageni hali inaonesha mvutio wa mazingira ya wekezaji iliyopo nchini na miradi 85 ni upanuzi wa uwekezaji wa awali hali inayodhihirisha imani si tu kwa wawekezaji wapya bali wa ndani,” alisema Rais Samia alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Julai 29, 2024 Ikulu Dar es Salaam.
Serikali yakanusha madai ya kuminya vyombo vya habari
Uchumi wa Tnazania kukua
Serikali yajipanga kukabiliana na taarifa za uzushi kuelekea uchaguzi