Fursa nne zilizojificha, matumizi ya nishati safi ya kupikia
- Ni pamoja na uzalishaji, usambazaji, na biashara ya kaboni.
Dar es salaam. Wakati mamia ya Watanzania wakihamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia Serikali imebainisha fursa zilizojificha katika nishati hiyo ambazo zinaweza kuwaingizia watumiaji wake kipato.
Mhandisi Anita Ringia, kutoka Wizara ya Nishati ameiambia Nukta Habari mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa fursa hizo za nishati safi zinaweza kutengezwa kwa urahisi kupitia mazingira yanayotuzunguka.
“Wajasiriamali pia wanaweza kunufaika kupitia uzalishaji wa bidhaa za nishati safi kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mazingira wanayo ishi, ikiwemo mabaki ya vifuu vya nazi, mabaki ya mkaa na rasilimali nyingine zinazoweza kutumika kutengeneza mkaa mbadala pamoja na majiko banifu” alisema Ringia.
Kauli ya Mhandisi huyo inakuja wakati ambapo Tanzania imebakisha miaka nane tu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa mwaka 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mpaka sasa utekelezaji huo umefikia asilimia 28.6, Serikali ikiongeza nguvu zaidi kuwafikia wakazi wa vijijini ambapo elimu ya matumizi ya nishati hiyo bado haijafika.
Ringia anasema ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo ni vyema jamii ichangamkie fursa iliyopo katika mnyororo wa thamani wa nishati hiyo ili kujiingizia kipato na kuokoa maisha ya Watanzania 33,000 wanaokadiriwa kupoteza maisha kutokana na matumizi ya nishati zisizo salama.

Fursa katika uzalishaji
Kulingana na takwimu hizo za matumizi ya nishati safi nchini Tanzania ni wazi kuwa zaidi ya asilimia 71.4 bado haijafikiwa hivyo kutoa fursa kwa wazalishaji wa nishati safi za kupikia ikiwemo mkaa mbadala, majiko banifu, makaa ya mawe, na gesi.
Ikiwa wajasiriamali hao wataongeza uzalishaji na kuyafikia maeneo ya vijijini ni wazi kuwa lengo la kupaisha matumizi ya nishati safi hadi asilimia 80 mwaka 2024.
Fursa katika usambazaji
Baada ya mchakato wa uzalishaji kukamilika ni lazima nishati hiyo isafirishwe kutoka eneo moja hadi kuwafikia watumiaji wake walioko maeneo mbalimbali nchini na kuwafikia ni lazima vyombo vya usafiri vihusike.
“usambazaji wa bidhaa za nishati safi, ambapo makampuni yanayozalisha gesi ya kupikia na yale yanayozalisha mkaa mbadala wamekua wakihitaji mawakala wa kusambaza bidhaa hizo hadi maeneo ya vijijini” alisema Ringia.

Fursa katika biashara ya kaboni
Ringia amebainisha kuwa nishati safi inaweza kufungua fursa katika biashara ya kaboni (carbon trading), ambapo miradi inayochangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa inaweza kupata mapato kupitia uuzaji wa carbon credits katika soko la kimataifa.
Alifafanua kuwa nchi zilizoendelea zenye viwanda vikubwa ambazo zimefikia ukomo wa viwango vya uzalishaji wa hewa chafu hununua ‘carbon credits’ kutoka kwenye miradi inayosaidia kuhifadhi mazingira katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Kwa upande wa sekta ya habari, Ringia alisema waandishi wa habari na watengenezaji wa maudhui mtandaoni (content creators) wana nafasi muhimu ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia
“watengeneza maudhui na waandishi wa habari wanayo fursa kubwa ya kutoa elimu na kutengeneza maudhui ya uelimishaji kupitia vipaji na majukwaa yao, tutumie hayo kutoa elimu na kuwaelimisha watanzania waweze kufahamu kwanini watumie nishati safi ya kupikia,” amesema Ringia.