Wanafunzi wanasayansi waibuka na suluhu wadudu waharibu nyumbani, shambani

December 20, 2021 4:28 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kutumia bidhaa za asili zinazotokana na wanyama na mimea.
  • Kati yake ni siagi na mmea ambao hupandwa kama maua nyumbani.
  • Afua hizo zimefanya kazi dhidi ya viroboto, mende, kunguni na mbu.

Dar es Salaam. Bila shaka ndoto ya kila mvumbuzi ni kutoa suluhu ya matatizo yanayoikabili jamii ili kuboresha maisha ya watu kwa kutumia njia rahisi za kiteknolojia.

Hata hivyo, suluhu hizo hazimfikii kila mtu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mfumo maalum wa kuzifikisha kwa wananchi, ukosefu wa elimu na kutoendana au kukubali kwa haraka mabadiliko ya njia za utendaji wa mambo kwenye jamii na gharama kubwa za suluhu husika.

Pamoja na changamoto hizo, kila siku wavumbuzi na wabunifu hasa vijana waliopo shuleni na mtaani wamekuwa wakiibuka na suluhu mbalimbali kuisaidia jamii yao kuwa na ustawi mzuri. 

Miongoni mwa eneo lililopewa kipaumbele katika suluhu hizo ni sekta ya kilimo na ufugaji ambapo wanafunzi kutoka shule mbalimbali nchini wanakutanishwa katika jukwaa la taasisi ya  Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) ili kuwasilisha suluhu zao na kusaidia kuzibiresha ili zikubalike kwenye jamii.

Hivi karibuni, jukwaa hilo liliendesha mashindano ya kuwatambua na kuwapa zawadi wanafunzi wenye suluhu bora yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ili kuvutia wanafunzi wengi kupenda masomo ya sayansi.

Miongoni mwa suluhu zilizowasilishwa katika mashindano hayo ni zile zinazolenga kuboresha kilimo, ujenzi na mazingira:

Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Ndoleleji ya mkoani Simiyu, Iddy Luchagula (kulia) na Sara Kija (kushoto). Picha| Rodgers George.

Siagi, mkombozi kwa wafugaji wa kuku

Magonjwa ya kuku ni miongoni mwa changamoto kubwa inayowasumbua sana wafugaji wa wanyama hao hasa wanapovamiwa na wadudu kama viroboto.

Endapo kuku akiandamwa na viroboto, inaweza kusababisha hadi kifo kutokana na ugonjwa wa tetekuwanga (fowl pox).

Wafugaji hutumia njia mbalimbali ikiwemo mafuta ya taa na mafuta ya mgando ya kupaka kukabiliana na ugonjwa huo lakini njia hizo zimethinitishwa kuwa siyo salama na zinaweza kusababisha changamoto zaidi kwa kuku.

Utafiti uliofanywa na wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Ndoleleji ya mkoani Simiyu, Iddy Luchagula na Sara Kija umebaini kuwa, matumizi ya mafuta ya taa kukabiliana na viroboto husababisha kuku kutokwa na damu sehemu ambazo hazina manyoya ikiwemo sehemu ya kichwa.

“Mafuta ya taa yanaua viroboto ndiyo lakini kuku anabaki na majeraha,” amesema Luchagula.

Kwa upande wa mafuta ya kupaka mwilini, wanafunzi hao wamebaini ya kuwa hayana msaada kabisa kumkinga kuku na maradhi ya wadudu hao.

“Mafuta ya mgando yanamsababishia kuku joto na baada ya kupakwa kichwani, yanaongezewa kemikali na harufu ambazo siyo nzuri kwa kuku,” amesema Kija.

Suluhu waliyoibua wanafunzi hao ni matumizi ya siagi inayotokana na maziwa ya ng’ombe. Kuitumia, unampaka kuku aliyeathirika na viroboto na kisha kusubiri matokeo.

Kija amesema, kuku akipakwa siagi hiyo katika sehemu yenye viroboto, huwakosesha hewa viroboto na hivyo kufa mara moja.

“Ni rahisi kupata hasa katika jamii ya wafugaji na hayana madhara kabisa kwa kuku,” amesema Kija.

Muonekano wa maua ya commelina yakiwa yamepandwa kwenye nyumba ya maboksi iliyotumika katika utafiti. Picha| Rodgers George.

Maua ya kufukuza wadudu

Kwa muda sasa mimea imekuwa ikitumika kama afua ya wadudu wa nyumbani na hata mashambani. 

Kuanzia mchaichai kama mmea wa kufukuza mmbu hadi mmea wa “commelina” ambao wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Nganza ya Mkoani Mwanza, Ester Massawe na Rachel Akyoo wamesema mmea huu kupandwa nyumbani unafukuza wadudu ikiwemo mbu na nzi.

Ester amesema, “unaweza kuchukua majani ya mmea huu na kuyaponda ponda kisha kuyaloweka kwenye maji kwa siku mbili. Baada ya hapo ukaweka kwenye chombo cha kunyunyiza vimiminika (spray bottle) na kupilizia ndani ya nyumba.

Katika utafiti wao walifanya majaribio kadhaa ya kupulizia maji ya commelina kwa wadudu kama viwavi, mende na kunguni na walikufa mara moja, na kubaini hiyo ni njia rahisi kwa watu kukabiliana na wadudu nyumbani.

Endapo elimu hii itawafikia wengi, watasahau gharama za kununua dawa za mbu nyumbani ambazo gharama yake inaanzia Sh2,000 kwa boksi.

Siyo hilo tu, maji yenye commelina yanaweza kutumika shambani kuua wadudu waharibifu ikiwemo viwavi na nondo.


Soma zaidi


Hawataishia hapa, ni mwanzo

Licha ya kuwa washindi wa tafiti hizi wamezawadiwa tuzo na zawadi, huu kwao ni mwanzo tu katika safari yao ya sayansi. 

Wadau wa sekta hiyo wamesema watawaweka kwenye darubini zao na kuwaendeleza kwa kuwasimamia na kuwaonyesha njia ya kupita ili waendeleze tafiti zao na kuwa na mchango mkubwa kwa jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu amesema wanafunzi hawo tayari ni wabunifu na hivyo wanahitaji kuendelezwa kwa kujengewa uwezo zaidi wa kuziendeleza kazi zao ili ziifikie jamii kwa urahisi.

“Watapatiwa mafunzo. Mafunzo hayo ni pamoja na kuangalia haki bunifu ambazo mtu anapobuni, vitu gani uvilinde ili usije ukaibiwa ubunifu wako,” amesema Dk Nungu.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Dk Amosi Nungu (katikati) akikabidhi kombe kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Dr Salmin Amour walioibuka washindi kwenye mashindano ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania. Wa kwanza kushoto ni Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kijamii kutoka kampuni ya Shell Tanzania Msomisi Mbenna, wa kwanza kulia ni Afisa Mtendaji wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee (KJF) Caren Rowland. Picha |YST.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Nukta TV

Mama Salama alivyombana Wanu kuhusu maslahi ya walimu wanaojitolea

Mama Salama alivyombana Wanu kuhusu maslahi ya walimu wanaojitolea

Nukta TV

Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Nukta TV