Tutatoboa: Wakazi wa Geita wanavyopambana kuung’oa ujinga
- Wachangishana zaidi ya Sh19,000 kujenga shule.
- Bado wana matumaini licha ya kuisubiria Serikali kumalizia madarasa.
- Mmoja asubiria shule ya sekondari kwa miaka 40.
Mbogwe. Shitulu Nghanza, mkazi wa kata ya Bunigonzi mkoani Geita, kwa miaka 40 alikuwa akitamani siku moja eneo lao liwe na shule ya sekondari kusaidia watoto wao kusoma karibu na nyumbani.
Hata hivyo, ndoto yake hiyo haikutimia kwa haraka kama alivyokuwa ametarajia, jambo lililompunguzia matumaini ya kuwa ipo siku watoto wao watapata elimu kama wenzao katika maeneo ya karibu.
Katika kipindi hicho cha miongo minne, watoto wa kata hiyo iliyopo wilayani Mbogwe, wamekuwa wakienda kusoma shule za kata za jirani hata baada ya hamasa ya kujenga shule za sekondari kuongezeka nchini miaka 15 ya hivi karibuni.
Sasa ndoto ya Nghanza na wakazi hao wameamua kuondoa adha ya watoto wao kusafiri umbali mrefu kufuata elimu.
“Ni usumbufu mkubwa kwa watoto, wakifaulu darasa la saba wanapangiwa shule za mbali na wengi wao wanashindwa kumaliza kidato cha nne,” anasema Nghanza.
Kata hiyo yenye wakazi 7,018 ina shule za msingi tatu za Ngezi, Bunigonzi na Mwabukwalule. Watahiniwa wa darasa la saba wanaofaulu katika shule hizo hupelekwa Shule ya Sekondari ya Isangijo iliyopo kata ya jirani ya Ushirika.
Mwanafunzi hulazimika kutembea kwa miguu kwa saa nne au kutumia baiskeli ambapo ni umbali wa kilomita nane kutoka kata ya Bunigonzi.
Fortunata Nungula, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Isangijo yeye hutumia baiskeli kwenda shule lakini si siku zote usafiri huwa imara.
Pale baiskeli inapoharibika, anasema hutembea kwa miguu hadi shuleni takriban kilomita nane na kumfanya achelewe masomo au kupewa adhabu.
“Wakati mwingine umeambiwa na walimu urudi shule Saa 10 jioni kwenda kusoma…mpaka urudi nyumbani inakuwa ni usiku sana, unaweza hata ukapata matatizo mbalimbali kama vile kubakwa, hii huwa inanifanya wakati mwingine nifikirie hata kuacha shule,” anasema Fortunata.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 15 anasema changamoto hizo zinatishia elimu yake kwa sababu hata masomo hafanyi vizuri.
Sehemu ya boma la shule ya sekondari ya Bunigonza ambayo itasawaondolea wanafunzi hadha ya kusafiri umbali mrefu. Picha| Gift Mijoe.
Kutokana na changamoto hizo, wakazi wa Kata ya Bunigonzi wameamua kujenga shule ya sekondari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
“Watoto wanasoma lakini hawamalizi shule, wanapata mimba zisizokusudiwa,” anasema Mtendaji wa Kata ya Bunigonza, Sabas Joel bila kutaja idadi ya wanafunzi waliopata mimba miaka ya hivi karibuni.
Takwimu za msingi za elimu za Tanzania (BEST) mwaka 2020 zilizotolewa na Ofisi ya Rais-Tamisemi zinabainisha kuwa mwaka 2019 pekee wanafunzi wa sekondari 5,398 nchini walipata ujauzito huku mkoa wa Geita ukiwa na wanafunzi 229.
Geita ulikuwa ni miongoni mwa mikoa 11 yenye idadi kubwa ya wanafunzi wa sekondari wenye ujauzito.
Mbogwe ilikuwa na wanafunzi wenye ujauzito 20 ikiwa ni ya nne kati ya halmashauri sita za mkoa huo wa kanda ya ziwa.Joel anasema walianza kuijenga shule hiyo ambayo iko kijiji cha Bunigonzi mwaka 2020 na mpaka sasa wamekamilisha maboma ya vyumba vitano vya madarasa, ofisi moja ya walimu na nyumba moja ya mwalimu.
“Majengo hayo yako usawa wa lenta na tumejenga kwa nguvu za wananchi kwa michango na wadau wa maendeleo,” amesema Joel na kwamba wanaisubiri Serikali ikamilishe sehemu iliyobaki ili wanafunzi waanze kusoma mwaka 2022.
Namna walivyohamasishana kujenga shule
Licha ya kuwa Serikali ina wajibu wa kutoa huduma za kijamii ikiwemo kujenga shule, Mwenyekiti wa kijiji cha Bunigonzi, Amosi Mgodagula anasema walifanya hamasa kubwa kwa wananchi kuwahimiza kujenga shule hiyo na muitikio ulikuwa mzuri.
“Tukaazimia kuchangia Sh19,500 kila mtu huku wengine wakitoa mifuko ya saruji na kuleta mawe 10 kila mmoja,” anasema Mgodagula aliyepo kwenye kamati ya ujenzi wa shule hiyo.
Ujenzi wa maboma ya shule hiyo ikijumuisha ofisi na nyumba ya mwalimu ambayo kukamilika kwake kutawapa tabasamu wakazi hao umegharimu Sh14.1 milioni.
Miongoni mwa vilivyowahamasisha wakazi hao ni elimu ya kujitambua na uraghabishi waliyopata kutoka kwa shirika la Tamasha kwa kushirikiana na Mtandao wa Waraghibishi wa Wilaya ya Mbogwe (MBODANET) iliyolenga kuwaamsha na kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo katika maeneo yao bila kuisubiri Serikali.
“Waraghibishi walikuja kwenye kata yetu na walitoa elimu kwa watu wachache ambao wakatoa hamasa kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya kata,” anasema Maria Welelo, mraghibishi katika kata ya Bunigonzi ambaye alipata mafunzo hayo mwaka 2017.
Bado matumaini kibao
Wazazi wa kata hiyo wana matumaini makubwa kuwa ikiwa shule hiyo itafunguliwa mwaka 2022 itasaidia kuwapunguzia gharama za kuwasomesha watoto shule za mbali.
“Tunaiomba Serikali itusaidie kupaua sekondari yetu ili watoto wasiwe wanahangaika kwenda mbali,” amesema Mkazi wa kijiji cha Shibutwe, Yustina Nyanda ambaye anasema wakati mwingine mtoto wake hutumia Sh7,000 kwa usafiri wa bodaboda kwenda shuleni.
Wazazi hao, ambao sehemu kubwa ni wakulima, wana matumaini kuwa shule hiyo itawapunguzia gharama za kuwapangia nyumba (mageto) watoto wao ili wakae karibu Bunigonzi.
Boma la shule ya sekondari inayojengwa na wakazi wa Bunigonza kwa ajili ya watoto wao. Picha| Gift Mijoe.
Baadhi ya wazazi wameiambia Nukta kuwa mageto huwaweka mbali watoto na uangalizi wao na kuwatumbukiza katika makundi hatarishi ya ngono na dawa za kulevya.
“Wale wasichana wanaokaa mtaani hawana elimu rika wanarubuniwa na vijana na kupata ujauzito na wa wavulana wanaingia kwenye makundi mabaya na kuacha shule,” anasema Diwani wa kata ya Ushirika wilayani Mbogwe, Deogratius Shayo.
Ukosefu wa shule ya sekondari katika kata ya Bunigonzi umefanya shule ya jirani izidiwe na wanafunzi kiasi cha kupunguza ufanisi wa kujifunza.
Shayo anasema ujenzi wa shule ya Bunigonzi utasaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika shule ya Isangijo kwa sababu inahudumia wanafunzi wa kata tatu ikiwemo ya Ngemo.
Kibarua kwa Serikali kumalizia shule
Nguvu kazi za wakazi hao wa Bunigonzi hazitakuwa zimezaa matunda iwapo Serikali itashindwa kumalizia shule hiyo kwa wakati.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imesema imetenga fedha kumalizia baadhi ya maboma wilayani humo katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/22.
“Kuanzia Julai mwaka huu kama fedha zitawahi, kwa kawaida fedha zinakuja kuanzia mwezi Septemba tunaamini itakwenda kutatua changamoto hiyo katika maeneo hayo ambayo wananchi wametoa nguvu zao,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Pastory Mukaruka.
Hata hivyo, anasema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha wananchi na wadau wa maendeleo wanajenga shule mpaka hatua ya mwisho bila kuisubiri Serikali ili kuondoa changamoto ya maboma mengi kukaa kwa muda mrefu bila kukamilika.
Latest