Tunachokifahamu kuhusu meli kubwa kuliko zote Ziwa Victoria
- Meli hiyo itakuwa kubwa zaidi ndani ya Ziwa Victoria ikiwa na uwezo wa kubeba watu 1,200, tani 400 za mizigo na magari madogo 20 kwa wakati mmoja.
- Itakuwa ikifanya safari zake hadi Uganda na Kenya.
- Serikali inatarajia meli hiyo itachochea ukuaji wa uchumi hasa baada ya kukamilika kwa mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Mwanza. Hatimaye Serikali imefanikiwa kuishusha majini meli mpya itakayokuwa ni kubwa kuliko zote ndani ya Victoria ya Mv.Mwanza “Hapa kazi tu” baada ya ujenzi wake kukamilika kwa hatua ya pili ya asilimia 82.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 92.6, kimo cha mita 20 na upana wa mita 17 imeshushwa leo February 12, 2023 ikiwa ni miaka minne tangu ilivyoanza kujengwa Januari 2019 jijini Mwanza.
Hadi kukamilika kwake, meli hiyo itakuwa na uzito wa tani 3,500 ikiwa ni ongezeko la tani 500 zaidi kutoka tani 3,000 zilizorekodiwa leo wakati ikishushwa majini ndani ya Ziwa Victoria.
Baada ya kukamilika na kuanza safari, meli hiyo itakuwa kubwa kuliko zote katika Ziwa Victoria.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya huduma za meli nchini (MSCL) Erick Hamis ameeleza leo baada ya zoezi la ushushaji wa meli hiyo kukamilika kuwa kilichofanyika ni hatua muhimu ya pili katika ujenzi wa meli hiyo.
Amesema sehemu kubwa ya ujenzi wa meli hiyo imefanywa na Watanzania kwa asilimia 100 wenye umri wa kati ya miaka 21 hadi 35 ambao walishirikiana na wakandarasi sita (6) kutoka nje ya nchi.
‘Bado kidogo ikamilike’
Hamis amesema hatua ya tatu ya ujenzi huo itakuwa ni kufanya majaribio, kupaka rangi kuweka vifaa vya kuongozea meli, kazi ambayo itadumu kwa muda wa kati ya miezi mine hadi mitano.
“Mpaka hapa ilipofikia tunaweza kusema meli imekamilika na hiyo asilimia 18 iliyobaki ni ukamilishaji wa mambo madogomadogo tu ambayo yatafanyika kwa kipindi kisichopungua miezi minne,” amesema Hamis.
Ujenzi wa meli hiyo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh109 bilioni kupitia fedha za walipa kodi.
“Mpaka sasa mkandarasi amelipwa zaidi ya bilioni 93.8 na kwa sasa serikali ndiyo inamdai kazi na atakapoikamilisha kiasi kilichobaki atapatiwa,” amesema Hamis.
Baada ya meli hiyo kukamilika, bosi huyo amesema wataalamu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) watakagua na kutoa chetu cha ubora na itakuwa kifanya safari zake kati ya Bandari za Bukoba, Kemondi, Jinja na Portbell nchini Uganda, Kisumu nchini Kenya, Musoma na Mwanza.
Meli ya MV. Mwanza “Hapa Kazi Tu” ikielea ndani ya Ziwa Victoria Februari 12, 2023 katika bandari ya Mwanza Kusini baada ya kushushwa majini kutokana na kukamilika kwa awamu ya pili ya ujenzi wake kwa asilimia 82. Meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo tani 400 na magari madogo 20. Picha|Mariam John/Nukta.
Tunachokifahamu hadi sasa kuhusu meli ya Mv. Mwanza
Meli hiyo ya Mv. Mwanza ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari madogo 20.
Ndani kutakuwa na madaraja sita yatakayoanza na daraja la VVIP litakalokuwa maalum kwa viongozi wa kitaifa ambao watakuwa wanakaa watu wawili tu wakati daraja linalofuata la VIP litabeba watu mashuhuri likihusisha watu wanne tu yaani vyumba vine.
Daraja la kwanza litahudumia watu 60, daraja la biashara litakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 100 na daraja la pili litakalokuwa na watu 200.
“Daraja la mwisho kwenye meli hii litakuwa ni la uchumi ambalo litakuwa minabeba abiria 834 na katika daraja hili kutakuwa na hadhi ya kisasa na wananchi watakaa kwa starehe na wataweza kufanya utalii,” amesema Hamis.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete akibonyeza kitufe kitakachoifanya meli ianze kuelea majini kwa ajili ya hatua ya tatu ya ykamilishaji. Picha|Mariam John/Nukta.
Ni mwendo wa burudani, lift kwa watu wenye ulemavu
Ndani ya meli hii pia kutakuwa na buradani mbalimbali na kutakuwa na sehemu ya lift hasa kwa watu wenye changamoto ya kupanda ngazi na wagonjwa, na sehemu ya hospotali (dispensary) na sehemu ya kina mama wajawazito.
“Tunatarajia meli hii itakuwa inatumia saa 10 pekee kwenda bandari ya Portbell nchini Uganda lakini pia itaenda Musoma mkoani Mara,” amesema Hamis.
Hata hivyo, nauli ya meli hii zitafahamika baada ya kukamilika na kupewa cheti cha ubora na Tasac.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema Serikali iliamua kujenga meli kubwa ili kukidhi mahitaji ya soko ambayo yanatarajiwa kuongezeka hasa baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Kujengwa kwa meli hiyo, amesema kutasaidia kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha safari mpya zitakazosaidia kurahisisha shughuli za kibiashara, kikazi, utalii na safari binafsi kwenye maeneo mengi zaidi ilivyo sasa.
Waziri huyo pia amepongeza kitendo cha kampuni hiyo kwa kutoa fursa za ajira kwa vijana wengi wakitanzania ambapo takribani watanzania 3,000 waliajiriwa katika mradi huu pamoja na chelezo lililotumika kujenga meli hiyo.
Mbali na hao, Watanzania wengine 2,000 wameajiriwa kwenye miradi mingine ya ukarabati wa meli.

Latest