TRA yatangaza mfumo mpya wa usajili wa magari, leseni za udereva

February 19, 2025 7:59 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Mfumo huu utawawezesha watumiaji kujihudumia wenyewe.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa usajili wa vyombo vya moto na utoaji wa leseni za udereva unaotarajiwa kurahisha utoaji wa huduma hizo nchini.

Taarifa ya TRA  iliyotolewa leo Februari 19, 2025 inabainisha kuwa mfumo huo wa kisasa wa usimamizi wa kodi za ndani unaojulika kama IDRAS umeanza kazi tangu Februari 10 mwaka huu ukiwawezesha watumiaji kujihudumia wenyewe kwa kutumia Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN)

“Mfumo huu unampatia nafasi mlipakodi kujihudumia mwenyewe (Self Services) kwa kuingia katika mfumo kwa kutumia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kupata mawasiliano ya ujumbe mfupi kwa njia ya simu (SMS) na barua pepe (e-mails)…

…Kufuatia hilo taarifa za Namba ya Utambulisho wa mlipakodi zinatakiwa kuwa na taarifa sahihi ili kuwezesha mawasiliano na kupata huduma kwa ukamilifu katika mfumo huo,” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na kitengo cha huduma kwa mlipa kodi.

Miongoni mwa taarifa muhimu za TIN zinazotakiwa kuwa na usahihi ni pamoja na namba ya simu na barua pepe (email) inayotumiwa na mwenye TIN, alama za vidole na picha (Biometrics) kwa TIN za watu binafsi na taarifa nyingine za TIN.

Mfumo huu unatarajiwa kuanza kutumika kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza, utahusisha moduli za usajili na usimamizi wa magari na vyombo vingine vya moto pamoja na utoaji wa leseni za udereva.

Aidha, Mamlaka hiyo imesema kupata huduma mbalimbali za mfumo, mtumiaji anatakiwa kuwa na akaunti ya kumwezesha kuufikia na kutumia mfumo huo kupitia Taxpayer Portal. 

Huduma katika mfumo mpya 

Miongoni mwa huduma muhimu zitakazopatikana na kufanywa na watumiaji kwa njia ya kielektroniki katika mfumo huo mpya ni mmiliki wa chombo cha moto kufanya usajili mwenyewe wakati anapoingiza gari toka nje ya nchi au kuinunua hapa nchini.

Mfumo huo pia utamuwezesha mmiliki wa gari au chombo kingine cha moto kuhamisha umiliki kwenda kwa mtu au taasisi nyingine, kubadili taarifa mbalimbali za chombo mabadiliko yanapotokea pamoja na waombaji wapya wa leseni kupata taarifa za kukamilika kwa ombi lake. 

Ili kuweza kuzifikia huduma mbalimbali za usimamizi wa vyombo vya moto na leseni za udereva, TRA imewataka walipa kodi na umma kwa ujumla kuzingatia kuhuisha taarifa za TIN ili kuwezesha kuingia katika mfumo na kupata taarifa mbalimbali juu ya huduma hizo. 

Iwapo mtu atakuwa hana uelewa juu ya taarifa ya TIN, TRA imemkumbusha kutembelea tovuti ya TRA (www.tra.go.tz) kupata mwongozo wa kuhuisha taarifa za TIN kwa njia ya kieletroniki.

Mambo mengine ya kuzingatia ni kufanya uhamisho wa umiliki wa magari na vyombo vingine vya moto ili viwe katika TIN na jina la mmiliki wa sasa na hivyo kuwezesha kutambulika na kupata huduma ikiwemo bima, stika za mapato, uhamisho wa umiliki (transfer of ownership) katika siku za usoni  

Sanjari na hayo TRA imeonya kuwa kushindwa kuhuisha taarifa za TIN na kuhamisha umiliki wa gari au chombo kingine cha moto kutasababisha kushindwa kupata huduma muhimu za magari na maombi ya leseni za udereva. 

Pia TRA wamesema kuwa, mifumo imeimarishwa na ofisi zake nchi nzima zimejipanga kuwawezesha walipakodi na umma kwa ujumla kupata huduma kwa urahisi. 

Miongoni mwa mambo muhimu katika kuwawezesha wamiliki kupata huduma TRA inatafakari utoaji wa misamaha ya riba na adhabu kwa waliochelewa kufanya uhamisho wa umiliki wa vyombo vya moto na miamala mingine. 

Kwa maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kuhuisha taarifa za TIN na kufungua akaunti katika taxpayer portal, mtumiaji anatakiwa kutembelea tovuti ya TRA www.tra.go.tz au kufika katika ofisi yoyote ya TRA iliyo karibu nae.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks