TRA yajivunia mafanikio haya miaka minne ya Rais Samia
- Ni pamoja na ongezeko la mapato na uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema inajivunia mafanikio iliyoyapata katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo kuongeza wigo wa ukusanyaji wa kodi ndani ya kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan.
TRA imepewa mamlaka kisheria kukusanya mapato yatokanayo na kodi ambayo ndio hutumika kuendesha shughuli mbalimbali za Serikali ikiwemo miradi ya maendeleo, huduma za kijamii pamoja na mishahara ya watumishi wa Serikali.
Yusuph Mwenda Kamishna Mkuu wa TRA aliyekuwa akizungumza leo Machi 12, 2024 na wanahabari jijini Dodoma amebainisha kuwa miongoni mwa mafanikio waliyopata ndani ya miaka minne ni pamoja na kuongeza makusanyo ya kodi kwa asilimia 78.

“Katika kipindi cha miezi nane ya mwaka wa fedha 2024/2025, TRA imekusanya Sh21.2 trilioni ikilinganishwa na Sh11.2 trilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho kabla ya Rais Samia kuingia madarakani, ikiwa ni ongezeko la asilimia 78,” amesema Mwenda.
Mwenda ameongeza kuwa mafanikio mengine ni mamlaka hiyo kujenga mahusiano imara na viongozi wa wafanyabiashara, viongozi wa dini pamoja na viongozi wa kijamii na wasanii wanaosaidia kutoa elimu ya ulipaji wa kodi kwa wananchi.
Katika kukabiliana na changamoto za walipakodi Mwenda amesema mamlaka hiyo imetenga siku ya Alhamisi kila wiki kwa ajili ya kukutana na walipa kodi katika ngazi mbalimbali za wilaya, mikoa na makao makuu ya TRA.

Aidha, katika juhudi za kuwezesha biashara na uwekezaji, TRA imeshirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kurahisisha taratibu za uwekezaji kwa kuunda kamati maalum ya kushughulikia matatizo ya wawekezaji na kurahisisha utoaji wa misamaha ya kodi.
Mwenda ameeleza kuwa katika kipindi cha miezi nane iliyopita, TRA imelipa marejesho ya kodi (tax refunds) ya Sh1.2 trilioni kwa wafanyabiashara ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka Sh92.3 bilioni zilizolipwa hapo awali.
Kuimarisha uadilifu na weledi wa watumishi
Kwa mujibu wa Mwenda, TRA imeboresha maadili na uwajibikaji wa watumishi wake, hatua iliyosaidia kupunguza migogoro ya kikodi na kuimarisha ushirikiano na walipa kodi ambapo katika miaka minne watumishi 15 wamefukuzwa kazi.
Aidha, wengine sita wameshushwa mishahara na 12 wameshushwa vyeo kutokana na ukiukwaji wa maadili ya kazi huku watumishi 22 wakipewa onyo la maandishi.
Usimamizi wa kodi kwa mifumo ya Tehama
Mkurugenzi wa TRA amewaambia wanahabari kuwa mamlaka hiyo imewekeza zaidi ya Sh200 bilioni katika mifumo miwili mipya ya usimamizi wa kodi ukiwemo wa TANCIS utakao shughulikia na kurahisha biashara ndani ya nchi na mfumo wa IDRAS wa kodi za ndani ya nchi pia umeanzishwa kwa ajili ya usimamizi wa magari, leseni na kadi za umiliki wa magari kwa njia ya kidijitali.

Uboreshaji wa huduma kwa walipa kodi
TRA imeongeza idadi ya ofisi zake na watumishi kwa lengo la kuboresha huduma kwa walipa kodi.
Mwenda ameeleza kuwa wakati Rais anaingia madarakani TRA ilikuwa na watumishi 4,749 ambapo mpaka kufikia sasa kuna jumla ya watumishi 6,989 huku watumishi 1,596 wakiwa mbioni kuajiriwa ili kuweka idadi ya watumishi 8,585 ikiwa ni ongezeko la asilimia 80.
Lengo la kuongeza watumishi hao ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma zote kwa wakati na kwa usahihi katika maeneo yote ya nchi.
Mafaniko mengine yaliobanishwa na Mkurugenzi huyo ni kutambua na kuthamini walipa kodi, kusimamia usawa katika biashara, kutoa elimu kwa walipa kodi, kuimarisha mfumo wa usimamizi wa kodi kwa lengo la kuongeza uwazi na kupunguza migogoro ya kikodi.
“Nimshukuru sana mheshimiwa Rais ameunda tume ya kutathimini mfumo wa kodi, sisi tutashirikiana naye kuhakikisha tunatengeneza mfumo wa kodi ambao kwanza unatabilika, mfanyabiashara akiwa kwake ajue anatakiwa kulipa kodi kiasi gani kwa wakati gani na muda gani yeye mwenyewe,’’ amebainisha Mwenda.
Awali, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa aliwaambia wanahabari kuwa kwa sasa Serikali inatarajia kuweka utaratibu wa kila taasisi kuelezea mafaniko yake ndani ya miaka minne ikiwa lengo ni kuwafanya wananchi kuelewa ni vitu gani vimefanyika.
Latest



