Rais Samia aagiza marekebisho mfumo wa haki madai
- Maboresho hayo yatasaidia kupunguza muda wa kusubiri hukumu.
- Ataka Mahakama kutumia mfumo wa usuhishi zaidi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu ameagiza kufanyika kwa marekebisho katika mfumo wa haki madai ili kupunguza ucheleweshaji wa haki unaofanyika katika ngazi mbalimbali zinazohusika kutoa haki nchini.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza na wahudhuriaji wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria yaliyofanyika Januari Mosi, 2024 jijini Dodoma amesema kulegalega kwa mfumo huo hufanya watumishi kupoteza muda huku ukiminya upatikanaji wa haki nchini.
“Hii inachukua muda mwingi kwa wadau wanaohusika kwenye mashauri haya na wanapoteza muda wa kufanya mambo mengine kwenye jamii kwa hiyo na huko niombe kutupiwe jicho kufanyiwe marekebisho na haki iweze kupatikana,” amesema Rais Samia.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mashauri yanayopita katika Mahakama ya wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi huchukua mwaka mmoja kusikilizwa hadi kukamilika kwa hukumu.
Zinazohusiana:Rais Samia : Simamieni haki kuimarisha imani ya mahakama Tanzania
Hali ni mbaya zaidi kwa Mahakama Kuu ambapo ili kesi ikamilike na hukumu itolewe utalazimika kusubiri hadi miaka miwili jambo linalozorotesha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Maagizo hayo ya kuboresha mfumo wa haki madai yanakuja wakati Serikali ikisubiri mpango kazi rasmi utakaosaidia utekelezaji wa ripoti ya tume ya haki jinai iliyokabidhiwa Rais Saamia Julai 15 mwaka jana na Mwenyekiti watume hiyo , Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman ikilenga kuboresha taasisi za jinai ikiwemo mahakama.
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa wakati maboresho hayo yakifanyika ni vyema Mahakama itumie mfumo wa usuluhishi ili kupunguza wingi wa madai na kuwawezesha wananchi na watoa huduma kuendelea na shughuli nyingine muhimu.

Wageni mbalimbali pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiwa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria Ddoma.Picha|Ikulu Mawasiliano.
Kesi za kibiashara zipewe kupaumbele
Rais Samia pia ameitaka mahakama kuharakisha hukumu zinazowahusu wafanyabiashara na wawekezaji ili kuwawezesha kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi zinazochangia katika ukuaji wa pato la Taifa
“Mwekezaji anathamini sana muda, kwani muda ni mali. Hapa namaanisha mwekezaji wa ndani na wa nje, na ndio maana ni lazima mitazamo ya wadau wa mahakama nchini ijielekeze kwenye kupunguza muda unaotumika kwenye mashauri…
…ili wananchi watumie muda wao kwingine kwenye masuala ya uzalishaji,” amesema Rais Samia.
Maagizo hayo ya Rais yanaenda sawa na Katiba ya Tanzania ibara ya 17a inayoanisha kanuni zinazotaka kutochelewesha haki bila sababu ya msingi pamoja na kutenda haki kwa wote kwa usawa.