Rais Samia: Mahakama itachochea utekelezaji dira mpya ya maendeleo 2050
- Asema dira mpya itachochea ukuaji wa uchumi hivyo mahakama ijiandae kutoa huduma za haki kwa wakati.
Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mahakama ya Tanzania itakuwa na mchango katika kuiwezesha nchi kufikia malengo ya maendeleo kama yalivyobainishwa kwenye Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kuweka mifumo bora ya kisheria na inayoendana na wakati.
Dira hiyo inayotoa mwongozo wa malengo na mwelekeo wa maendeleo ya nchi kwa miaka 25 ijayo itaanza kutekelezwa mwaka huu hadi mwaka 2050 baada ya ile ya awali kuisha muda wake.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika mkoani Dodoma leo Februari 3, 2025 amesema kuwa dira hiyo itavutia ongezeko la mitaji ya uwezekezaji nchini hivyo mahakama na sekta zote za haki madai zijiandae vyema.
“Utekelezaji wa dira utavutia mitaji ya uwekezaji jambo litakalohitaji kuingia mikataba mbalimbali baina ya Serikali na sekta binafsi. Hivyo, natoa rai kwa sekta zote zinazohusika na haki madai kujiandaa vyema katika kutoa huduma za haki,” amesea Rais Samia.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.Picha|Ikulu.
Kutokana na umuhimu wa suala hilo Rais Dk Samia ameitaka Mahakama ya Tanzania na Mabaraza ya Mashauri ya Kodi kuwa wawezeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa kutenda haki kwa usawa na kwa wakati.
Aidha, Rais Samia ameitaka mahakama kujiandaa kukabiliana na changamoto za fedha za kidigitali (cyptocurrency) ambazo zitaenda kuongezeka kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
“Tunapokwenda katika miaka 25 ijayo, Tanzania itakuwa sehemu ya dunia inayoelekea kupunguza matumizi ya fedha taslimu mkononi, kuelekea mfumo wa ‘cashless nation’…
…Lakini pia, tunakabiliwa na changamoto za fedha za kidijitali kama cryptocurrency na mifumo mingine ya fedha za mtandaoni. Hili linatufanya tujipange kwa umakini mkubwa kuhakikisha mfumo wa sheria unakuwa tayari kukabiliana na mabadiliko haya,” amesema Rais Samia.
Katika kulinda masilahi ya Taifa katika sekta ya fedha na uchumi Rais Samia amemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha mikataba yote inayosainiwa na Serikali na mashirika yake inafanyiwa tathmini kwa umakini mkubwa.
“Kikatiba, ofisi yenye dhamana ya upekuzi na tathmini ya mikataba ya serikali ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ili kuhakikisha mikataba hiyo inalinda masilahi ya taifa, ni lazima watumishi wa ofisi hiyo wawe na uelewa wa kina wa masharti ya mikataba ya kiuchumi na uwezo wa kusimamia utekelezaji wake,” amesisitiza Rais Samia.
Aidha, ametoa wito kwa wataalamu wa sheria kuhakikisha mifumo ya kisheria inaimarishwa ili kuendana na mabadiliko makubwa yanayotarajiwa katika sekta za fedha na uchumi katika miongo ijayo.
Pia Samia amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya Mahakama, kama ilivyoshauriwa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Boniface Mwabukusi.