TMA yatoa tahadhari ya kimbunga Jude
- kitaingia eneo la nchi kavu katika eneo la Msumbiji leo
- Kitapungua nguvu kabla ya kurejea tena Machi 13 hadi 15 mwaka huu.
Arusha. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa kimbunga Jude katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji ikiwataka watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka mamlaka hiyo.
Taarifa ya TMA iliyotolewa leo Machi 10, 2025 inabainisha kuwa kimbunga hicho kitaingia eneo la nchi kavu katika eneo la Msumbiji leo na baadae kupungua nguvu kabla ya kurejea tena Machi 13 hadi 15 mwaka huu.
“Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu katika eneo la Msumbiji mchana wa leo tarehe 10 Machi 2025 na kupungua nguvu yake…
…Hata hivyo, Kimbunga “Jude” kinatarajiwa kurejea tena baharini na kuimarisha nguvu yake katika kipindi cha kati ya tarehe 13 hadi 15 Machi 2025.,” imesema taarifa ya TMA.
Hii ni mara ya pili ndani ya mwaka 2025 TMA kutoa tahadhari ya vimbunga katika bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu yanayopakana na pwani ya bahari hiyo.
Januari 14, mwaka hu TMA ilitahadharisha umma juu ya ujio wa kimbunga Dikeledi kilichotarajiwa kusababisha hali ya mbaya ya hewa katika mikoa ya pwani ya kusini ikiwemo Lindi na Mtwara.
Hata hivyo, Kimbunga hicho hakikusababisha madhara makubwa Tanzania zaidi ya vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa ambavyo vilitabiriwa kukoma kuanzia tarehe 16 Januari, 2025.
Pamoja na taarifa hiyo, TMA imesema kutokana na mwelekeo na umbali wake Kimbunga Jude hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja hapa nchini zaidi ya kuchagiza mifumo ya hali ya hewa na kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali.
Vilevile, uwepo wa kimbunga hicho unaendana sambamba na kuanza kwa msimu wa mvua za Masika, 2025 katika maeneo yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka kama ilivyotabiriwa awali na taarifa kutolewa kwa Umma mnamo tarehe 31 Januari 2025.
Katika hatua nyingine TMA imewashauri watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka mamlaka hiyo pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga Jude na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.
Latest



