TMA yaeleza suluhisho la upatikanaji wa maji, akiadhimisha siku ya hali ya hewa

March 23, 2020 9:58 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kwa sasa watu takribani bilioni 2.2 wanakosa maji ya kunywa na bilioni 4.2.
  • Imesema mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya mzunguko wa maji kwa namna tofauti tofauti. 
  • Taarifa sahihi za hali hewa zitasaidia mikakati ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Dar es Salaam. Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD), siku ambayo jumuiya ya hali ya hewa duniani kote inaadhimisha kumbukizi ya siku ambayo mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa Machi 23, 1950. 

Kwa kawaida siku hii huadhimishwa na kila nchi mwanachama wa WMO ambapo kwa Tanzania inaratibiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Hali ya Hewa na Maji”.  

Kaulimbiu hiyo inaenda sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2020, ambayo imejikita katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye sekta ya maji. 

Maji yanagusa kila sekta duniani, upatikanaji wake una umuhimu mkubwa katika kuendesha maisha na shughuli za binadamu lakini mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa ni yanatatiza katika upatikanaji wa maji safi na salama.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), iliyotolewa jana (Machi 22, 2020) kuhusu maendeleo ya maji  inatahadharisha kuwa mabadiliko ya tabianchi yataathiri uwepo, ubora na kiasi cha maji yanayohitajika kwa matumizi na haki ya msingi ya binadamu kutumia maji safi na salama ya kunywa na usafi. 

Ripoti hiyo inaeleza kwa sasa watu takribani bilioni 2.2 wanakosa maji ya kunywa na bilioni 4.2 huku asimilia 55 ya idadi ya watu ulimwenguni, wanakosa mfumo wa uhakika wa kujisafisha kwa maji. 

Hali hii inaongeza ugumu wa kufanikisha lengo namba sita kati ya malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya 2030 (SDGs) ambalo linalenga kuuhakikishia ulimwengu upatikanaji wa maji kwa gharama nafuu ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa takwimu za UNESCO, matumizi ya maji yameongezeka mara sita katika karne iliyopita na yanaongezeka kwa kiwango cha asilimia moja kila mwaka. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaonekana kwa kuongezeka kwa mzunguko na kasi ya hali mbaya ya hewa (dhoruba, mafuriko, ukame, joto) na kuongeza tatizo la maji duniani.

Maji yamekuwa sehemu muhimu ya maisha ya binadamu lakini mabadiliko ya hali ya hewa yanatishia upatikanaji wa rasilimali hiyo. Picha|Mtandao.

TMA yafafanua uhusiano wa hali ya hewa na maji

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, DK Agnes Kijazi katika ujumbe wake wa Siku ya Hali ya Hewa Duniani amesema ongezeko la joto duniani linasababisha changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na limeathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya mzunguko wa maji kwenye uso wa dunia kwa namna tofauti tofauti. 

“Kwa mfano, maeneo yenye joto zaidi hupata mvukizo zaidi wa maji kutoka baharini, ziwani, ardhini na kwenye mimea. 

“Hivyo, anga lililopo katika eneo lenye joto zaidi lina uwezo wa kuhifadhi unyevunyevu kwa asilimia nne  zaidi kwa kila ongezeko la nyuzi joto moja katika kipimo cha “Celcius”, na kupelekea kufanyika kwa mawingu ng’amba ambayo huambatana na mvua kubwa na ngurumo,” amesema Dk Kijazi. 

Ongezeko la joto husababisha mvukizo wa maji kutoka kwenye udongo na kufanya ardhi kuwa kame zaidi na udongo kuwa mgumu kwa sababu maji kushindwa kuingia kwenye udongo pindi mvua inaponyesha, badala yake maji hutiririka kukimbilia kwenye mito, maziwa na baharini, na kuiacha ardhi kuendelea kuwa kame. 

“Matokeo yake ni uwezekano wa kuongezeka kwa matukio ya ukame na upungufu wa maji safi na salama,” amesema bosi huyo wa TMA.

Aidha, ongezeko la joto katika maji ya mito, maziwa, bahari na mabonde ya maji husababisha uhaba wa hewa safi ya oksijeni kwenye maji na kupelekea vifo kwa viumbe hai ambao hutegemea hewa hiyo. 

Hali hiyo inaonyesha wazi kuwa hali ya hewa ina mchango mkubwa katika mtawanyiko na upatikanaji wa maji katika uso wa dunia, pamoja na ubora wa maji yanayohitajika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu.

Hata hivyo, Dk Kijazi ambaye ni Makamu wa tatu wa Rais wa WMO amesema pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na athari zake katika mfumo wa mzunguko na upatikanaji wa maji, taarifa za hali ya hewa za sehemu husika zitasaidia katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea upatikanaji wa maji. 

Taarifa hizo ni pamoja na data za hali ya hewa za kipindi kirefu (klaimatolojia), utabiri wa hali ya hewa na matazamio ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate change projections) ambazo zitasaidia kufanya maamuzi sahihi ya upatikanaji wa maji. 


Soma zaidi: 


Serikali kuiongezea nguvu TMA

Katika kuhakikisha kuwa TMA inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, Serikali imesema inaendelea kuijengea uwezo ili iweze kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa lengo la kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa. 

“Serikali imeendelea kuongeza uwezo wa TMA kwa kuboresha mtandao wa Taifa wa vituo vya upimaji wa hali ya hewa ili kuboresha upatikanaji wa data na usahihi wa utabiri wa hali ya hewa,” amesema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe katika ujumbe wake wa Siku ya Hali ya Hewa Duniani. 

Amezitaka mamlaka za maji nchini kuzingatia taarifa na ushauri wa hali ya hewa unaotolewa na TMA kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana ili kuimarisha shughuli za maendeleo.

“Sekta ya maji izitumie huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango yao ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu,” amesema Mhandisi Kamwelwe. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW