TMA: Viwango vya usahihi wa utabiri wa hali hewa vyaongezeka Tanzania
- Vimefikia asilimia 93 juu ya asilimia 70 vinavyokubalika kimataifa.
- Utabiri wa hali ya hewa unasaidia kufanya maamuzi sahihi.
Dar es Salaam. Katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Samia Suluhu Hassan, viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa vimeongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 93, jambo linalosaidia katika maamuzi ya sekta mbalimbali Tanzania.
Kiwango cha usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ni asilimia 70.
“Ongezeko hili la usahihi wa utabiri unazifanya huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kuwa za uhakika na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta zote za kiuchumi na kijamii nchini,” imeeleza taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani.
Aidha, mamlaka hiyo imeendelea kutoa utabiri wa msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa usahihi na ubora hivyo kuchangia kupunguza athari kwa watu na mali zao.
Mathalan, Oktoba 2021, TMA ilitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli kuwa chini ya wastani hivyo kuwezesha mamlaka mbalimbali kufanya maamuzi stahiki na kusaidia kuepusha madhara makubwa ambayo yangeweza kutokea.
“Kutokana na kujengewa uwezo na serikali katika nyanja za miundombinu, teknolojia na wataalam, Mamlaka imeanza kutoa utabiri wa msimu kwa ngazi ya wilaya ambao umekuwa na mwitikio mkubwa na watumiaji wengi,” imeeleza TMA katika taarifa hiyo.
Soma zaidi:
- TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa
- Watanzania washauriwa kutumia taarifa za hali ya hewa kwenye mipango ya maendeleo
- Ujio mfumo wa taifa wa hali ya hewa kuchochea ujenzi wa viwanda nchini
Mambo yaliyochangia kuimarika kwa usahihi wa utabiri
Katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Samia, mamlaka hiyo imefanikiwa kufanya ununuzi wa rada mbili za hali ya hewa ambazo zitakamilisha lengo la muda mrefu la kuwa na rada saba za hali ya hewa nchi nzima.
“Rada hizo zinatarajiwa kufungwa mkoani Dodoma na Kilimanjaro. Uundwaji wa rada mbili za hali ya hewa zinazotarajiwa kufungwa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya unaendelea kufanyika kiwandani nchini Marekani,” imeeleza TMA.
Mamlaka imefanikiwa kununua kompyuta ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuchambua taarifa za hali ya hewa na hivyo kuipa uwezo wa kutoa utabiri maalum kwa maeneo madogo madogo.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Mamlaka imefanya malipo ya vifaa vya kupima matukio ya radi (lightning detectors) vitakavyofungwa katika maeneo yenye matukio ya mara kwa mara ya radi.
Vifaa vingine vipo katika hatua mbalimbali za ununuzi ikiwemo vifaa vya kuandaa utabiri wa hali ya hewa na mitambo nane ya kutoa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga.
Pia mitambo 13 ya kupima hali ya hewa mahsusi kwa sekta ya kilimo, vifaa 10 vya kupima upepo na vifaa 60 vinavyojindesha vyenyewe kwa ajili ya kupima kiwango cha mvua.
Taarifa sahihi za hali ya hewa husaidia kufanya maamuzi sahihi katika sekta mbalimbali za utendaji hasa kilimo ambapo wakulima huzitumia kufahamu ni mazao gani walime na kwa wakati gani.