Thamani ya hisa kampuni mbili soko la hisa Dar yashuka

October 21, 2019 2:10 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wawekezaji wa kampuni ya bia ya Afrika Mashariki (EABL) na kampuni ya habari ya NMG leo watalala na maumivu baada ya thamani ya hisa za kampuni hizo kushuka kwa viwango tofauti.
  • Thamani ya hisa za kampuni ya NMG imeshuka kwa asilimia 5.26 huku za EABL ikishuka kwa asilimia 0.47.

Dar es Salaam. Wakati thamani ya mauzo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiongezeka kwa asilimia 35.7, wawekezaji wa kampuni ya bia ya Afrika Mashariki (EABL) na kampuni ya habari ya NMG leo watalala na maumivu baada ya thamani ya hisa za kampuni hizo kushuka kwa viwango tofauti 

Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Oktoba 21 inaeleza kuwa  thamani ya mauzo ya soko hilo hadi linafungwa leo jioni ilikuwa Sh525.4 kutoka Sh337.7 iliyorekodiwa mwisho wa juma Oktoba 18, 2019. Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 35.7.

Wiki za DSE hujumuisha siku za kazi pekee yaani Jumatatu hadi Ijumaa.

Wakati thamani ya mauzo katika soko hilo ikipaa, thamani ya hisa za NMG imeshuka kwa asilimia 5.26 ambapo wawekezaji wake wamepoteza Sh50 kwa kila hisa moja. 

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa  thamani ya hisa moja ya NMG ilikuwa ni Sh900 kutoka Sh950 iliyorekodiwa ijumaa.

Kampuni nyingine ambayo thamani ya hisa zake imeshuka ni EABL ambayo imeporomoka kwa asilimia 0.47 huku kampuni hiyo ikipoteza Sh20 kwa kila hisa moja.Hadi soko linafungwa thamani ya hisa moja ya EABL ilikuwa Sh4,240 kutoka 4,260 iliyorekodiwa ijumaa.


Zinazohusiana: 


Wakati wawekezaji wa kampuni hizo mbili wakiugulia maumivu, wenzao wa benki ya KCB wana kila sababu ya kutabasamu baada ya thamani hisa zake kupanda kwa asilimia 1.06 huku kampuni nyingine zikibaki katika viwango vilivyokuwepo ijuma zikiwemo Vodacom, benki ya CRDB, DCB na Acacia. 

Hata hivyo, benki ya CRDB ndiyo iliyofanya vizuri zaidi leo baada ya kuongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa. 

CRDB imeuza hisa 515,940 sawa na asilimia 81.5 ya hisa zote zilizouzwa sokoni leo huku ikifuatiwa kwa mbali na NICO ambayo imeuza hisa 63,000 na kampuni ya bia ya TBL (50,948).

Enable Notifications OK No thanks