Teknolojia, uvumbuzi kwenye kilimo kupunguza umaskini Tanzania

September 17, 2019 11:55 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ripoti mpya ya Benki ya Dunia imezitaka nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kuongeza kasi ya uvumbuzi kwenye kilimo na matumizi ya teknolojia ili kumaliza umaskini.
  • Imeeleza kuwa uwekezaji mpya unahitajika ili kuongeza maarifa mapya na kuhakikisha uzalishaji katika sekta ya kilimo unaongezeka sambamba na ukuaji wa kipato cha watu.

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Benki ya Dunia imezitaka nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kuongeza kasi ya uvumbuzi kwenye kilimo na matumizi ya teknolojia kwa wakulima ili kumaliza umaskini, kukidhi ongezeko la mahitaji ya chakula na kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa, 

Ripoti hiyo ya Teknolojia na Ukuzaji wa Uzalishaji katika kilimo  iliyotolewa jana (Septemba 17, 2019) Jijini New York, Marekani, inaeleza kuwa kukwama kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo hasa katika nchi za Asia Kusini na Afrika ambako idadi kuwa ya maskini wanaishi kunazuia juhudi za kuboresha maisha ya watu waishio vijijini. 

Imeeleza kuwa uwekezaji mpya unahitajika ili kuongeza maarifa mapya na kuhakikisha uzalishaji katika sekta ya kilimo unaongezeka sambamba na ukuaji wa kipato cha watu.

 “Karibu asilimia 80 ya watu (watu wanane kati ya 10) maskini duniani wanaishi katika maeneo ya vijijini. Ili kupunguza umaskini, kuna haja ya kujikita katika kuongeza uzalishaji katika kilimo; sekta ambayo ina mchango mkubwa wa kupunguza umaskini takriban mara mbili zaidi ya uzalishaji viwandani,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Benki ya Dunia. 

 Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia ukuaji, Fedha na taasisi, Ceyla Pazarbasioglu ameeleza katika uzinduzi wa ripoti hiyo kuwa kama uzalishaji kwenye kilimo utaongezeka, utazalisha ajira nyingi na fursa mbalimbali mjini. 

Amesema ili kufikia azma hiyo, yanahitajika mabadiliko makubwa ya mfumo wa uvumbuzi kwenye kilimo, matumizi mazuri ya fedha za umma pamoja na kuwepo kwa mnyororo wa thamani wa mazao ya wakulima ili kumfaidisha kila anayeshiriki katika sekta hiyo. 

“Teknolojia mpya inaboresha upatikanaji na gharama za habari, fedha na bima katika sekta zote ikiwemo kilimo. Hii inaweza kusaidia kuongeza uzalishaji kwa wakulima wenye ujuzi mdogo, lakini inawezekana tu ikiwa kuna motisha na uwezo mzuri wa kukuza na kuendeleza teknolojia hiyo, ” amesema Pazarbasioglu. 


Zinazohusiana: 


Hii ni mara ya nne kutolewa kwa ripoti hiyo inayotathmini vichocheo na vizuizi vya uzalishaji kwenye kilimo na kutoa ushauri wa kisera unaohitajika katika sekta hiyo inayotegemewa na watu wengi zaidi duniani. 

Hata hivyo, ripoti hiyo imeeleza kuwa mavuno ya mazao Asia Mashariki yameongezeka mara sita katika miongo minne iliyopita, na kuchangia kupungua kwa umaskini nchini China na nchi zingine za ukanda huo.

Kwa Afrika na baadhi ya maeneo ya Asia ya Kusini mavuno yameongezeka mara mbili tu, jambo linalorudisha nyuma juhudi za kupunguza umaskini katika maeneo hayo.  

Pia, ripoti imebainisha kuwa juhudi za kutumia teknolojia ziende sambamba na kutatua changamoto za mabadiliko ya hali hewa hasa ukame ili kuiwezesha dunia kuzalisha chakula kitakachokidhi mahitaji ya wakazi wake.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW