TADB yakusudia kujenga kiwanda cha kuchakata chai Iringa

March 11, 2019 11:26 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kiwanda hicho kitafungua milango ya fursa kwa wakulima kutumia teknolojia ya kisasa za kulima na kuongeza uzalishaji na soko la zao hilo. 
  • TADB na wadau wengine watasaidia kuboresha na kuendeleza ardhi ya wakulima inayohitajika kwa kilimo cha zao hilo. 

Dar es SalaamHuenda wakulima wa chai mkoani Iringa wakafaidika na uzalishaji wa zao hilo, baada ya Benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) kuonyesha nia ya kusaidia utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa chai katika wilaya ya Kilolo kwa kuwezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuboresha mashamba ya wakulima. 

TADB kwa kushirikia na wadau wa maendeleo wanakusudia kujenga kiwanda cha kuchakata chai kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.

Mradi wa kuendeleza zao la chai unatekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Chama cha Wakulima wa Chai cha Dabaga (Datega) na Kampuni ya Chai ya Kilolo (KTC) ambapo Datega pekee inamiliki ardhi ya hekta 3,600 yenye haki miliki ambayo ni fursa kwa vitalu vya kuotesha miche ya chai, uanzishaji wa mashamba na usindikaji wa chai na kilimo cha miti ya mbao.

Kutokana na fursa hiyo, TADB inakusudia kuanzisha kiwanda cha uchakataji wa chai katika wilaya hiyo ili kusaidia usindikaji wa chai inayolimwa na wakulima wa Kilolo ambao kwa muda wanategemea zao kama shughuli yao ya kibiashara. 

Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo (Machi 11, 2019), inaeleza kuwa ili kufanikisha mradi huo wawekezaji wanaalikwa kushirikiana wadau wa chai ili kuwezesha ujenzi wa kiwanda hicho kwa kusambaza vifaa vya uzalishaji, vitendea kazi na teknolojia itakayofungua fursa na kukuza thamani ya zao la chai wilayani humo.

Katika kutekeleza mradi huo, benki hiyo itatoa msaada wa kifedha, kuchangia katika uboreshaji na utanuzi wa shamba lenye ukubwa wa hekta 184 lililopo sasa. 

“Msaada wa kifedha wa TADB utajumuisha kuwaendeleza wakulima wadogo wa chai wafaidike na fursa ya kuongeza uzalishaji kutoka hekta 170 zilizolimwa chai hadi kekta 13,600,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 


Soma zaidi: viwanda vya kuchakata mbaazi kufufua matumaini ya soko kwa wakulima Tanzania


TADB pia itasimamia uanzishwaji na uendeshaji wa malighafi zinazohitajika katika uanzishaji wa kiwanda hicho na kuanzisha shamba la miti kwa ajili ya upatikanaji wa nishati ya kuendesha kiwanda.

Wakulima na kampuni ya KTC nao watasaidiwa kutumia teknolojia rahisi ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama za uendeshaji. 

Wakulima wa Kilolo watapata fursa ya kutumia teknolojia ya kisasa ambayo itawawezesha kuongeza uzalishaji na kupata tija kwenye kilimo cha chai. Picha| Mtandao.

Mwekezaji atakayeingia katika mradi huo, atatakiwa kutengeneza miundombinu ya uchakataji yenye uwezo wa kuchakata walau kilo 30,000 za zao la chai kwa mfululizo wa siku 300 ambapo mradi huo ni lazima uhusishe wakulima wadogo na hata wakubwa moja kwa moja.

Pia, mwekezaji atatakiwa kuwekeza katika vifaa vya manunuzi na usafirishaji vitakavyosaidia usafirishaji wa mazao kutoka mashambani hadi eneo la kuchakata ikiwa ni pamoja na usimamizi na masoko.

Jukumu lingine ni kuanzisha maeneo ya kukuzia mbegu na kutoa mafunzo na ujengaji uwezo kwa wakulima pamoja na kuanzisha mashamba darasa kwenye vijiji 26 ambavyo vinapatikana wilayani humo.

Chai ni miongoni mwa mazao ya biashara ambayo yanaliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2017 cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambapo mwaka 2017 iliingiza Sh108. bilioni ikiwa mbele ya pamba ambayo iliingiza Sh80.2 bilioni. 

Enable Notifications OK No thanks