TASAC:Tumeanza kuchunguza chanzo cha meli kuzama ziwa Victoria
- Uchunguzi huo utashirikisha wataalamu wabobezi wa masuala ya miundombinu ya meli, mitambo na mifumo ya uundaji wa meli.
Mwanza. Shirika la Uwakala wa meli Tanzania (TASAC) limeanza kufanya uchunguzi wa chanzo cha kupinduka na kuzama kwa Meli ya MV. Clarias ikiwa ni siku mbili tangu kutokea kwa tukio hilo jijini Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAC, Mohamed Salum aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza baada ya kutembelea eneo la tukio leo Mei 21, 2024 amesema ili kukamilisha uchunguzi huo watazungumza na wafanyakazi wa meli ikiwemo nahodha na mabaharia.
Soma zaidi:Kimbunga IALY kusababisha mvua, upepo kwa siku mbili Tanzania
“Baada ya kutembelea eneo la tukio tumeanza uchunguzi wa kitaalamu kubaini kilichosababisha meli kulalia upande mmoja kabla ya kuzama majini ikiwa imetia nanga Bandari ya Mwanza Kaskazini…
…Tutazungumza na wafanyakazi (nahodha na mabaharia) kufahamu meli ilikuwa na changamoto gani watusaidie kabla ya uchunguzi utakaohusisha chombo chenyewe,” amesema Salum.
Uchunguzi wa meli hiyo iliyojengwa mwaka 1961 utashirikisha wataalamu wabobezi wa masuala ya miundombinu ya meli, mitambo na mifumo ya uundaji wa meli.

Mwonekano wa meli ya Mv. Claries ikiwa inaonekana nusu mgongo baada ya kupinduka na kuzama ndani ya Ziwa. Picha na Mariam John/ Nukta
Juhudi za kuitoa meli ziwani zinaendelea
Salum amebainisha kuwa tangu kutokea kwa tukio hilo Mei 19, 2024 juhudi za kuitoa majini meli hiyo ya MV.Clarias zinaendelea ambapo Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) ikishirikiana na kampuni ya Songoro Marine na Mkombozi Transport zinashirikiana kuitoa meli hiyo.
“Sababu za kiufundi meli kuzama ni mashaka ya kufikirika, yawezekana ilikunywa maji (yaliiingia) ikiwa imetia nanga ikalalia upande mmoja,kwa nini iliingiza maji hicho ndicho tunachokitafuta,”amesema Salum.
Baada ya zoezi hilo kukamilika meli hiyo itapelekwa kwenye chelezo Mwanza Kusini kwa uchunguzi na watakachobaini kisha wataishauri Serikali hatua za kuchukua.