Rais Samia amfuta kazi Mkurugenzi Mkuu TPA
- Amesema utendaji wake ni wa kusua sua.
- Hali hiyo imekuwa kikwazo kwa wawekezaji na ukuaji wa biashara.
- Awataka waliokabidhiwa bandari wafanye kazi kwa kasi, kuwatupia macho.
Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kusema haridhidhwi na kasi ya utendaji wa bandari nchini, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus, nafasi ya Hamissi imechukuliwa na Plasduce Mbossa ambaye kabla alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
Rais Samia amechukua uamuzi huo muda mfupi baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Tabora hadi Isaka uliofanyika leo Julai 4, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi akizungumza katika hafla hiyo amesema haridhishwi na utendaji wa bandari za Tanzania kwa sababu kasi ya kuchangamkia fursa za wawekezaji ni ndogo, jambo linalokwamisha Tanzania kuwa kitovu cha biashara Afrika.
Rais Samia amesema Serikali imefanya juhudi mbalimbali kuboresha miundombinu ya usafirishaji kuchagiza biashara ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) lakini ufanisi wa bandari uko chini, jambo linalochelewesha nchi kufaidika kiuchumi.
“Wale tuliowakabidhi bandari zetu wafanye kazi kwa kasi mno. Siridhishwi kabisa na kazi za bandari, siasa zilizopo, longo longo zilizopo. Watu huko nje, bandari zinaendeshwa kwa kasi kubwa na biashara zinakua kwa kasi kubwa kupitia bandari zetu sisi bado tunasua sua,” amesema Rais Samia.
Amesema watendaji wa bandari wafanye kazi kwa bidii ikiwemo kuhakikisha wawekezaji wanaokuja nchini wanapatiwa huduma bora.
“Wawekezaji wanakuja ni kuzungushwa mwanzo mwisho, tutizame siasa, uchumi, tutizame sijui kitu gani. Nasema bandari watu wafanye kazi,” amesisitiza Rais Samia na kubainisha kuwa anakusudia kupitia upya shughuli za bandari nchini ili kuboresha utendaji wake.
Tanzania ina bandari mbalimbali kwenye maziwa na bahari ikiwemo ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza na Kigoma.
Zinazohusiana:
- Zanzibar, kitovu utengenezaji wa meli Afrika Mashariki
- Fundi mkuu wa kivuko cha Mv Nyerere aokolewa akiwa hai
- Bunge lahoji kutojenga bandari ya Bagamoyo
Amesema, mathalan bandari ya Dar es Salaam ndiyo jicho la Tanzania na ikifanya vizuri, nusu ya bajeti ya Serikali inayopangwa kila mwaka inaweza kutolewa na bandari hiyo.
Amesema ikiwa reli ya kisasa ya SGR ikiunganishwa vizuri na bandari ya Dar es Salaam kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Burundi, Tanzania itaweza kulifikia soko kubwa la Afrika.
Amesema lengo la kujenga reli ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha shughuli za biashara zinazofanyika katika bara hilo.
“Pamoja na miundombinu tunayoijenga ya bandari, reli, barabara na usafiri wa anga bado tuna kazi ya kujipanga ili kufaidika na fursa za kibiashara zilizopo ulimwenguni. Tukumbuke hatuko peke yetu tuko kwenye dunia ya ushindani.
“Tunaposema Dar es Salaam iwe kituo, ni kuchukua hatua haraka mwekezaji anapokuja,” amesema Rais Samia.
Aidha, ameitaka sekta binafsi kuchangamkia fursa zinazoambatana na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji itakayoongeza kasi ya biashara baina ya Tanzania na nje za nje.
Rais Samia alimteua Hamis kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA Aprili 2021 akichukua nafasi ya Mhandisi Deusdedith Kakoko aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema mpaka sasa thamani ya ujenzi wa SGR umefikia Sh16.7 trilioni baada ya kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kipande cha Tabora hadi Isaka.
Hadi sasa, Serikali imetoa Sh6.4 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo inayotoka Dar es Salaam hadi Mwanza na baadaye Tabora hadi Kigoma na kuunganisha nchi za jirani ikiwemo Burundi na Congo DRC.
Amesema ujenzi wa reli hiyo umetoa ajira takriban 16,000 zenye thamani ya Sh224 bilioni ambazo zimelipwa kwa watu wanaofanya kazi katika ujenzi huo.
Amesema reli hiyo ikijengwa itasaidia kuifanya Dar es Salaam siyo kuwa tu kitovu cha biashara bali mikoa ya Tabora na Mwanza itakuwa vituo vikubwa vya shughuli hizo Tanzania na nchi jirani.