Ahueni: Tanzania yapandisha kima cha chini cha mshahara 35.1% 

May 1, 2025 4:02 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Nyongeza hiyo itaongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Sh370,000 hadi kufikia Sh500,000.
  • Ongezeko hilo linatarajiwa kuanza rasmi mwezi Julai mwaka huu wa 2025.

Dar es Salaam. Huenda wafanyakazi wa umma Tanzania wakapata ahueni ya kiuchumi baada ya Serikali kutangaza kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi hao kwa  asilimia 35.1 kuanzia mwezi Julai mwaka huu. 

Uamuzi huo uliopokelewa kwa shangwe na maelfu ya wafanyakazi utasaidia kupoza machungu ya ongezeko la gharama za bidhaa na upatikanaji wa huduma ikiwemo mafuta.

Rais Samia aliyekuwa akihutubia Watanzania katika maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa mkoani Singida amesema kuwa nyongeza hiyo itaongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Sh370,000 hadi kufikia Sh500,000 kwa mwezi. 

Nyongeza hiyo itaongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Sh370,000 hadi kufikia Sh500,000. Picha | Ikulu

Rais Samia ameongeza  kuwa nyongeza hiyo haitagusa tu kima cha chini, bali ngazi nyingine za mishahara pia zitaboreshwa kwa kiwango kinachowezekana kulingana na bajeti ya serikali.

“Baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda na umepanda kwasababu ya nguvu zenu wafanyakazi, ninayo furaha kuwatangazia kwamba katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, serikali mwaka huu itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1…Ngazi nyingine za mshahara nazo zitapanda kwa kiwango kizuri jinsi bajeti inavyoturuhusu,” ameongeza Rais Samia.

Kwa upande wa sekta binafsi, Rais Samia amesema kuwa Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara inaendelea kufanya mapitio ili kuboresha viwango vya chini vya mishahara katika sekta hiyo. 

Aidha, Rais Samia amehimiza ushirikiano kati ya Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, vyama vya wafanyakazi na waajiri katika kuhakikisha mikataba ya hali bora ya kazi inatekelezwa kwa ufanisi.

“Pamoja na kazi inayofanywa na bodi hiyo, nimehimiza wizara na vyama vya wafanyakazi kufanya majadiliano na waajiri ili kutekeleza mikataba ya hali bora ya wafanyakazi katika sekta binafsi, waendane sambamba na wenzao wa sekta ya umma,” amesisitiza Rais Samia.

Pamoja na Rais Samia pia kuwaahidi wafanyakazi kuwa Serikali yake itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi yaoi kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu amewataka wafanyakazi na vyama vyao kuendeleza amani na kuepuka kutumiwa kisiasa.

“Ili kujenga Taifa letu ni lazima tulinde utulivu na amani nchini…Historia ya vyama vya wafanyakazi ni vyama vilivyoleta vuguvugu la uhuru wa nchi hii, tusijibadilishe tukawa vyama vya kusaliti uhuru wetu tulioutafuta kwa nguvu kubwa.” amesisitiza Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa wito kwa wafanyakazi kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu ili kutumia haki yao ya kikatiba.

Awali, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya ameipongeza Serikali kwa kutambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi. Amepongeza hatua ya Serikali kuongeza mafao ya wastaafu kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000 kwa mwezi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks