Rais Samia: Jitokezeni kuboresha taarifa zenu ili mpige kura
- Uboreshaji huo unafanyika katika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo Zanzibar.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kujiandikisha au kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ili watumie haki yao ya kikatiba ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba.
Hii ni awamu ya pili ya uboreshaji wa daftari hilo ambapo kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) unafanyika katika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania Zanzibar.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Mei 17, 2025 katika kituo cha kujiandikisha kilichopo Chamwino jijini Dodoma pamoja na kuwapongeza wananchi wanaoendelea kujiandikisha amesisitiza kutumia fursa hiyo kwa kuwa nafasi hiyo haitojirudia tena.
“Huu ni mzunguko wa pili, waambieni ambao hawakujitokeza katika mzunguko wa kwanza, tuko kwenye mzunguko wa pili. Tukikosa nafasi hii, mbele hatuna tena nafasi ya kurudia. Kwa hiyo ili usipoteze haki yako naomba wananchi wote wawahi kwenye mzunguko huu wa pili,” ameongeza Rais Samia.

Rais Samia ambaye awali alikuwa akipiga kura visiwani Zanzibar sasa atapiga kura Tanzania Bara kwa kuwa ni mkazi wa Chamwino jijini Dodoma mara baada ya kuboresha taarifa zake.
Wito wa Rais Samia unakuja ikiwa imesalia miezi mitano kuelekea uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais, ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakitashiriki uchaguzi huo.
Hata hivyo, Rais Samia amebainisha athari za wananchi kutojiandikisha akionya kuwa kufanya hivyo ni kujinyima haki ya kikatiba na kukosa fursa ya kuchagua kiongozi anayemuhudumia.

“Jiulize mwenyewe rohoni kwa uzalendo wako uko wapi? Hii ni fursa kubwa. Nenda kaandikishe, piga kura, weka kiongozi unayehisi atakuhudumia,” amefafanua Rais Samia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 17,2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji Mwambegele, ilieleza kuwa uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa awamu ya pili utafanyika katika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania Zanzibar.
“Tunatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 1,396,609, kuboresha taarifa za wapiga kura 1,092,383, na kufuta wapiga kura 148,624 waliopoteza sifa,” alieleza Jaji Mwambegele.Hata hivyo, Mwambegele alisisitiza kuwa sambamba na zoezi hilo, INEC itaandaa daftari la awali la wapiga kura na kuliweka wazi kwa umma kama ilivyoelekezwa na kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria hiyo ya mwaka 2024.
Latest



