Tanzania yang’ara tena tuzo za eneo bora la utalii duniani

November 23, 2018 2:48 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link

Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka saba tokea mwaka 2011, raia wa Urusi kupitia jarida hilo wanaichagua Tanzania kama eneo bora zaidi la utalii. Picha|PlanetWare.


  • Imeshinda tuzo ya kuwa eneo bora la utalii duniani inayotolewa na Jarida la “National Geographic Magazine” la nchini Urusi kwa mwaka 2018.
  • Ni baada ya watu 263,000 kushirikishwa katika upigaji kura kwa njia ya mtandao, ikiwa ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka saba tokea mwaka 2011, Tanzania kupata tuzo hiyo.  
  • Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) nayo yajipanga kuitangaza zaidi Tanzania kimataifa.

Dar es Salaam. Tanzania inazidi kung’ara kimataifa, safari hii imeshinda tuzo ya utalii kwa kuonekana ni eneo bora zaidi la utalii duniani kwa mwaka 2018.

Tuzo hiyo ya kifahari katika sekta ya utalii inajulikana kama “The Best Destination to the World in the Category of Exotic Destination 2018” imetolewa na Jarida la “National Geographic Magazine” la nchini Urusi ambapo Tanzania imepata ushindi huo kutokana na kura zilizopigwa kwenye mtandao wa jarida hilo lililoshirikisha wapiga kura 263,000.

Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka saba tangu mwaka 2011, raia wa Urusi kupitia jarida hilo wanaichagua Tanzania kama eneo bora zaidi la utalii duniani.

Mwaka 2011, Zanzibar ilipata tuzo ya ‘Star Travel’ kama eneo bora zaidi la utalii wa ufukweni katika bara la Afrika na  mwaka jana Tanzania ilipata tuzo ya “National Geographical Travel” ikishika nafasi ya pili katika tuzo hizo.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeeleza kuwa juzi Novemba 21, 2018, Balozi wa Tanzania nchini Urusi Meja Generali, Simon Mumwi amepokea tuzo hiyo kutoka kwa uongozi wa jarida hilo jijini Moscow kwa niaba ya nchi.   

Mafanikio hayo yanatokana na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi Urusi, Wizara za Utalii za Tanzania Bara na Zanzibar, na Taasisi zote zinazosimamia masuala ya utalii za ndani na nje ya nchi katika kutangaza vivutio vya utalii kwa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Urusi.


Zinazohusiana: Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii

                          Mama Samia atoa maagizo matano kukuza utalii Tanzania


Tuzo hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii nchini ambapo idadi ya watalii wanaokuja Tanzania kutoka Urusi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Taarifa hiyo inaeleza kuwa  idadi ya watalii kutoka nchini humo imeongezeka kutoka watalii 4,021 mwaka 2012 hadi watalii 10,060 mwaka 2017.  

“Wizara kupitia Ubalozi wetu itaendelea kuongeza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na tunategemea kwa kushirikiana na wadau wengine katika juhudi hizi, idadi ya watalii kutoka Urusi wanaokuja nchini itaongezeka zaidi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati Tanzania ikijivunia hatua iliyopiga katika kukuza utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inatanua wigo wa kuongeza watalii katika masoko 18 ulimwenguni katika mwaka wa fedha wa 2018/19 baada ya kutangaza rasmi ratiba ya maonyesho 22 ya kimataifa inayoshiriki na kuratibu ikiwa ni fursa kwa kampuni za utalii nchini kusaka watalii zaidi je ya nchi.

TTB imebainisha kuwa maonyesho hayo 22 ambayo inashiriki yanafanyika katika nchi 18 kati ya Julai 2018 na Juni 2019. 

Maonyesho yaliyoangaziwa katika mwaka huu wa fedha ni yale yaliyopo katika nchi za Rwanda, Zimbabwe,  Ufaransa , Kenya, Canada, Uingereza, China, Hispania, Uholanzi na India. Mengine ni ya Marekani, Ubeligiji, Israeli , Afrika Kusini, Ujerumani, Urusi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Korea Kusini.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...