Mama Samia atoa maagizo matano kukuza utalii Tanzania

September 15, 2018 5:27 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Maagizo hayo ni pamoja na mikoa kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kufanya tamasha la Urithi Festival.
  • Miundombinu ya reli, anga na bandari kuimarishwa kuvutia watalii wengi kuingia nchini.
  • Urithi Festival itasaidia kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa lakini pia itaongeza mapato yasiyo ya kodi kwa Serikali.
  • Utamaduni wa Mtanzania na Malikale kupaishwa kimataifa.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo makuu matano yatakayosaidia kukuza sekta ya utalii nchini na kuongeza mapato yasiyo ya kodi ikiwemo mikoa kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kufanya maadhimisho ya tamasha la utamaduni la ‘Urithi Festival’ kila mwaka.

Mama Samia ametoa maagizo hayo leo (Septemba 15, 2018) wakati akizindua tamasha la Urithi Festival na kueleza kuwa utalii ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi ndiyo maana Serikali inawekeza kwa kiwango kikubwa ikiwemo katika kuboresha usafiri wa anga na reli.

Katika kuhahakisha unakua, ameiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuboresha miundombinu ya bandari  ili kuwezesha meli za kimataifa za kitalii kuingiza watalii wengi nchini ikiwa ni mkakati mwingine wa Serikali kutumia rasirimali zilizopo kuutangaza utamaduni wa Mtanzania.

“Mamlaka ya Bandari Tanzania izingatie sekta ya utalii kwa kujenga gati na majengo mahususi kwa ajili ya kupokea meli za watalii,” amesema Makamu wa Rais na kubainisha kuwa, “Jiji la Dar es Salaam lina fursa nzuri ya kupokea watalii wa meli lakini miundombinu ya bandari lazima iboreshwe.”

Amesema kuwa ulimwenguni kuna meli kubwa za kitalii ambazo zinabeba watalii hadi 6,000 ambapo zikija katika Bandari ya Dar es Salaam, Serikali itapata mapato na itafungua fursa kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa za kitamaduni.

“Nawaagiza Wakuu wa mikoa yote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha Urithi Festival inaadhimishwa katika mikoa yote Tanzania kila mwezi wa Septemba kuanzia mwaka ujao wa 2019 na kuendelea,” amesema Makamu wa Rais katika agizo lake jingine kwa mamlaka zilizopo chini yake.


Zinazohusiana:


Ukiachana na mikakati hiyo ndani ya Serikali, Mama Samia ametaka taasisi za umma kushirikiana kikamilifu na sketa binafsi na wananchi kufanya tamasha la Urithi Festival mikoani ili kuongeza wigo wa kuwafikia watu wengi zaidi.

Wizara ya Maliasili na Utalii yenyewe imeagizwa kuandaa mchakato wa kisheria utakaosaidia tamasha hilo kutambulika kisheria kwa sababu limeonekana kuimarisha na kudumisha umoja wa kitaifa kwa kuwaleta pamoja watu wa kada tofauti katika shughuli za maendeleo.

“Pili, naelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inaandaa taratibu ili Urithi Festival itambulike kisheria,” amesema.

Wizara hiyo, inayoongozwa na Dk Hamisi Kigwangalla, imeagizwa pia kutenga eneo mahususi ambalo itajengwa miundombinu rafiki kwa ajili ya maadhimisho ya kitaifa ya tamasha hilo la Urithi Festival.

Malengo ya Urithi Festival ni pamoja na kuimarisha, kuendeleza na kutangaza alama na tunu za taifa ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Pia ni chombo au sehemu muhimu ya kutangaza vivutio vya utalii na utamaduni wa Mtanzania ambao kwa muda mrefu haujatambulika katika nyanja za kimataifa.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (Kulia) akipokea zawadi ya picha kutoka kwa mmoja wa washiriki wa Tamasha la “Urithi Festival” lililozinduliwa leo Jijini Dodoma. Anayeshuhudia (nyuma) ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga. Picha| Urithi Festival

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema wizara yake inatambua umuhimu wa tamasha hilo na imejidhatiti kuhakikisha linafanyika kila mwaka katika maeneo mbalimbali ili kutimiza malengo ya Serikali ya kukuza mapato ya ndani na nje.

“Kazi ya kujenga nchi yetu na kuendeleza uhifadhi wa malikale ni kubwa,” amesema Hasunga na kuongeza kuwa mikakati iliyopo ni pamoja, “kuanzisha studio maalum kwa ajili ya matangazo ya utalii. Pia, tutaanzisha kituo cha chaneli za TV (televisheni).”  

Pia Serikali imeanzisha mfumo wa Tehama utakaoratibu shughuli zote za watalii wanaoingia nchini na kukamilisha kanuni za kuwasajili watoa huduma za utalii  ili kuboresha utoaji huduma hizo.

Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Urithi Festival kwa mwaka huu litaadhimishwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na visiwa vya Zanzibar ambapo shughuli zitakazofanyika katika tamasha hilo ni ngoma na muziki wa asili, mapishi ya vyakula vya kitanzania, maonyesho ya zana za utamaduni na vivutio vingine vya utalii.

Kuanzia mwaka 2019, Tamasha hilo litakuwa linaadhimishwa katika mikoa yote na linatarajiwa kufungua fursa mbalimbali kwa kampuni za utalii kuwekeza katika maeneo mbalimbali na wananchi kupata ajira za uhakika kuendesha maisha yao.

Katika mwaka 2017, sekata ya utalii ilileta watalii 1.5 milioni na kuliingizia Taifa Dola za Marekani 2.2 bilioni.Baadhi ya wasanii wakitumbuiza katika Tamasha la Urithi Festival lililofanyika katika uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma. Picha| Urith Festival.

Enable Notifications OK No thanks