Fedha za Uviko-19 zakamilisha jengo la ICU Bugando

July 6, 2022 7:01 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Jengo hilo jipya lina uwezo wa kupokea wagonjwa 15 kwa siku.
  • Ni Sh3.9 bilioni ambazo pia zimenunua vifaa tiba.
  • Litapunguza gharama za wagonjwa kusafiri hadi Dar es Salaa.

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda  Bugando imekamilisha ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) litakasaidia kupunguza changamoto ya wagonjwa wanaokumbwa na shida hiyo ambapo awali ilikuwa ikipokea wagonjwa wachache.

Hospitali ya Bugando imeshapokea kiasi cha Sh3.9 bilioni ambacho kimetumika katika ukarabati na ununuzi wa vifaa ambapo kwa upande wa ukarabati umekamilika kwa asilimia 100 huku vifaa tiba imekamilika kwa asilimia 90.

 Akizungumza katika sherehe ya upokeaji wa vifaa tiba na upanuzi wa chumba cha wagonjwa mahututi, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dk Fabian Massaga, amesema fedha za ukarabati ni sehemu ya mkopo wa Sh1.3 trilioni uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili kukabiliana na athari za Uviko-19.

Hospitali hiyo ilitengewa jumla ya Sh4.2 bilioni na  mpaka sasa wamepokea bilioni 3.9 ikiwa ni kwa ajili ya ukarabati wa ICU na ununuzi wa vifaa tiba na fedha iliyobaki Wizara ya Afya inakamilisha mchakato wa kuwanunulia gari la kisasa la kubebea wagonjwa na gari maalumu la kuhifadhia na kusafirisha damu.


Zinazohusiana:


Ujenzi wa ICU umekamilika kwa asilimia 100, na umegharimu Sh500 milioni.

“Ujenzi umejumuisha upanuzi wa ICU ya magonjwa ya ndani (medical), magonjwa ya upasuaji (surgical) na magonjwa ya watoto wachanga (neonatal) kabla ya maboresho tulikuwa na ICU yenye vitanda 12 kwa magonjwa yote ya ndani na upasuaji na vitanda 12 kwa watoto wachanga ila sasa hivi tutakuwa na  ICU yenye jumla ya vitanda 51(medical 11, surgical 19 na neonatal 21 na ujenzi umekamilika kwa asilimia 100 huku vifaa ni asilimia 90,” ameeleza Dk Massaga.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amesema vifaa vilivyowekwa ni vya kibobezi na kuutaka  uongozi wa hospitali hiyo pamoja madaktari na wauguzi kutoa huduma kwa kutafsiri ubobezi wa vifaa hivyo kwa vitendo katika kuwahudumia Watanzania.

Maboresho hayo yatapunguza changamoto za wananchi kusafiri hadi jijini Dar es Salaam kufuata huduma hizo.

“Ni mapinduzi makubwa katika sekta ya afya na zaidi katika kutokomeza vifo vinavyotokana na magonjwa mbalimbali, tumeshuhudia kuanza kwa huduma za kibobezi kwa ajili ya huduma za dharura na mahututi na kazi zimeanza,” amesema Mhandisi Gabriel.

Muuguzi Kiongozi  idara ya  wagonjwa mahututi ya watoto wachanga katika hospitali hiyo, Dk Sophia  Sembe amesema kuwa wameweza kupata jengo bora na zuri zaidi ambapo kwa sasa wanaweza kuhudumia wagonjwa wengi zaidi ambapo mwanzoni hawakuweza.

“Kwa sasa tunaweza kuwahudumia wagonjwa 21 kwa wakati mmoja wakati awali tuliweza kuhudumia wagonjwa 10 lakini kwa jengo bora na huduma bora tunahitaji rasilimali watu,  timu ya wauguzi wa kutosha na madaktari wabobezi ili tuweze kutoa huduma bora zaidi, tunaimani Serikali itafanyia kazi,” amesema Dk Sembe.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW