Tanzania yaangalia uwezekano wa kuwavuna mamba kuokoa maisha ya raia
Ongezeko la mamba kwenye mito ya maji limekuwa tishio kwa wananchi wanaotumia rasilimali hiyo kwa shughuli mbalimbali za maendeleo. Picha|Mtandao.
- Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amesema idadi yao imeongezeka sana katika maeneo mbalimbali na kutishia uhai wa wananchi.
- Mamba wamekuwa wakitumika katika shughuli za utalii.
Dar es Salaam. Serikali imesema inaangalia uwezekano wa kuwavuna mamba nchini katika mito mbalimbali iwapo wataonekana ni wengi kupindukia ili kupunguza athari wanazopata wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
Hatua hiyo inakuja baada ya kubainika kuwa mamba wamezaliana sana hasa katika Mto Ruvuma, jambo linalotishia uhai wa wananchi wanaotegemea rasilimali ya mito katika shughuli za maendeleo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa ufanunuzi huo Bengeni leo (Juni 18, 2019) wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Lulindi mkoani Lindi, Jerome Bwanausi aliyetaka kujua Serikali inachukua hatua gani kutatua changamoto ya ongezeko la mamba katika Mto Ruvuma linalotishia maisha ya wananchi.
Kanyasu amekiri kuwepo kwa ongezeko kubwa la mamba na wanyama wengine katika maeneo mengi nchini ambao hawatumiki moja kwa moja kuhamasisha utalii.
Amesema wamechukua hatua mbalimbali kuwalinda wananchi na ongezeko la mamba katika mto huo ikiwemo kuchimba visima ili wananchi wapate maji katika maeneo yao.
“Kwanza tulielekeza watu wetu wa TAWA (Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania), kuhakikisha wanapeleka visima vya maji katika vijiji ambavyo viko katika maeneo hayo.
“Lakini la pili tumewaagiza watu wetu wa TAWRI (Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania) kufanya utafiti na kutueleza mamba waliopo wamezidi kwa kiasi gani tuweze kuweka mkakati wa kuwavuna,” amesema Kanyasu.
Zinazohusiana:
- Kitulo ‘Bustani ya Mungu’ fahari ya Nyanda za Juu Kusini.
- Ijue milima 10 mirefu zaidi Tanzania.
- Ndani ya Ifisi: Hifadhi ya wanyamapori inayotoa pumziko kwa wakazi wa Mbeya.
Hata hivyo, Kanyasu amesema yuko tayari kwenda katika eneo la mto Ruvuma katika jimbo la Lulindi kuangalia hali halisi na kuzungumza na wananchi.
Katika swali lake Bwanausi amesema kwa kuwa uwepo wa mamba ni sehemu ya kivutio kwa watalii, lakini kumekuwa na ongezeko kubwa la mazalia ya wanyama hao katika Mto Ruvuma na kuleta athari kubwa kwa wananchi.
Amemtaka Naibu Waziri, Kanyasu kwenda katika jimbo lake na kutatua changamoto hiyo.
Mamba wamekuwa kivutio kikubwa cha utalii katika hifadhi za Taifa ikiwemo ya Rubondo na Saanane lakini wamekuwa chanzo cha vifo hasa kwa wananchi wanaoishi karibu na mazalia ya wanyama hao.
Kwa mujibu wa taasisi ya Crocodiles of the World ya nchini Uingereza, Afrika kuna mamba kati ya 250,000 hadi 500,000.