Namna ya kuwashawishi watu kupata chanjo
- Wape nafasi ya kuzungumzia uelewa wao wa chanjo ya Uviko-19.
- Toa taarifa sahihi kuhusu chanjo ikiwemo faida zake.
Dar es Salaam. Kampeni za utoaji chanjo dhidi ya Uviko-19 zinaendelea katika maeneo mbalimbali duniani kuhakikisha kuwa ugonjwa huo unatokomezwa na hauleti madhara zaidi kwa watu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia Oktoba 25, 2022, dozi za chanjo bilioni 12.8 zilikuwa zimesambazwa duniani kote.
Ni dhahiri kuwa chanjo ya Uviko-19 imepokelewa kwa namna tofauti kwenye jamii. Wapo ambao tayari wamechanja lakini wengine hawana mpango kabisa. Wengine wanasubiri watu wengi wachanje ndipo na wao waungane nao.
Ili watu wajitokeze kuchanja, wanatakiwa kuelimishwa kuhusu umuhimu wa chanjo kwa sababu inagusa moja kwa moja afya zao.
Zipo mbinu mbalimbali za kuzungumza na mtu kuhusu chanjo ya Uviko-19 hasa wasiotaka na wale ambao bado wanasita kufanya maamuzi.
Shirika la afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo ambao umeweka wazi njia nne za kuzungumza na mtu kuhusu chanjo ya Uviko-19:
Sikiliza kwa makini
Mpe nafasi mtu mtu mwenye wasiwasi kuhusu chanjo atoe maoni yake. Msikilize hoja zake bila kumpinga, kisha mueleza kwa kina kuhusu chanjo na faida zake.
Hakikisha unajibu maswali yake kwa ufasaha na kumuondolewa kila shaka aliyonayo ili kumfanya akubali kuchanjwa.
Ongea kwa utaratibu kuhusu Uviko-19 na watu wa rika tofauti.Picha | PBS.
Uliza maswali
Pia kuuliza maswali ya wazi kama vile “Umesikia nini juu ya chanjo za Uviko-19?”, maswali haya husababisha majibu zaidi ya “ndiyo” au “hapana” na yanaweza kukusaidia kuelewa vizuri shida za watu wanaotakiwa kupata chanjo. Pia inaweza kumsaidia mtu mwingine kufanya kazi kupitia mawazo yao.
Toa taarifa sahihi
Mpatie mtu taarifa sahihi na za kuaminika kuhusu chanjo ambazo zinatoka katika mamlaka za afya ikiwemo WHO. Kabla ya kuzungumza na mtu omba idhini yake ili kuepuka kuonekana unamshinikiza kuhusu kupata chanjo.
Kama huna majibu ya uhakika kuhusu swali uliloulizwa, usijibu badala yake tafuta taarifa za uhakika kuhusu jambo husika.
Tangazo:
Eleza faida za kupata chanjo
Wakati wa kujadili kuhusu chanjo, pia toa sababu zako za kutaka kupata chanjo na ikiwa uko katika nafasi nzuri eleza uzoefu wako jinsi itakavyosaidia kukinga familia na jamii na kurudisha shughuli na raha za maisha ambazo zilikuwepo kabla ya Uviko-19.
Hata hivyo, mashirika mbalimbali ndani na nje ya sekta ya afya yanaweza kuchukua jukumu muhimu katika kutoa habari sahihi juu ya chanjo na faida zake.
Hiyo inaweza kusaidia watu kujitokeza na kupata chanjo kwa wingi.
Pia mashirika hayo yanatakiwa kuongoza kwa mfano yaani kusaidia katika utoaji wa chanjo, kujenga uaminifu (kusikiliza maswali na kutoa ushauri kuhusu chanjo) na pia kusaidia katika kuvunja vizuizi vya aina yoyote juu ya chanjo.
Ikiwa watu wataelekezwa kwa ufasaha, uwezekano wa kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ni mkubwa.