Tanzania kuwakumbuka mashujaa wa vita vya Maji Maji

February 18, 2020 12:16 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Itawakumbuka katika maadhimisho yatakayofanyika Februari 22 hadi 27, 2020.
  • Wanafunzi wa shule watafunza umuhimu wa kutunza urithi wa Taifa na utamaduni.
  • Katika maadhimisho ya ya miaka 113 ya mashujaa wa vita vya Maji Maji, wafanyabiashara na wajasiriamali kupata jukwaa la maonyesho ya bidhaa zao.

Dar es Salaam. Shule 16 za mkoa wa Ruvuma zinatarajiwa kunufaika na mafunzo ya umuhimu wa kutunza urithi wa Taifa na utamaduni ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 113 ya mashujaa wa vita vya Maji Maji.

Mafunzo hayo yatafanyika kwa siku nne kuanzia Februari 22 hadi 25, 2020. 

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk Joel Lwoga amesema maadhimisho hayo yanalenga kuelimisha umma juu ya utamaduni na kutoa fursa kwa Watanzania kuenzi, kutunza na kuendeleza urithi, asili na utamaduni kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho kwani mpango huo ni endelevu.

“Ukiacha kwamba tunaenda kwenye shule 16, tuna mpango wa kuendelea kutoa mafunzo kupitia makumbusho ya Songea (mkoani Ruvuma) na makumbusho zingine zilizopo Tanzania,” amesema Dk Lwoga.

Pia amesema mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na vijarida ni kati ya mipango itakayotumika kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa urithi na utamaduni wa Kitanzania.

Naye Mwenyekiti wa kamati  ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Christine Ngereza amesema maadhimisho hayo yataambatana na shughuli zitakazofanyika kwa makundi kuanzia Februari 22 hadi kilele cha maadhimisho hayo Februari 27 ambapo mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme. 

Ngereza amesema shughuli hizo ni pamoja na kutembelea maeneo mbalimbali na kujifunza juu ya vita vya Maji Maji likiwemo pango ambalo Chifu Msaidizi Songea Mbano alikuwa anajificha wakati vita hivyo vikiendelea.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa  Dr Joel Lwoga (kati kati), Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Christine Ngereza (kulia) na Afisa Maonyesho Makumbusho ya Taifa, Balthazar Nyamusya (kushoto). Picha| Rodgers George.

Hata hivyo, maadhimisho hayo yatajibu maswali ya  wanafunzi na Watanzania ambao kwa mara zote wamekuwa wakiuliza juu ya kumbukumbu ya maji yaliyotumika kwenye vita hiyo kwani watapata majibu yao kwa mara ya kwanza kwenye maadhimisho hayo mwaka huu.

“Tumekuwa tukipata maswali kutoka kwa wanafunzi kwamba bado hamjatuonyesha ile dawa ya maji maji ilitengenezwaje. Mojawapo wa kitu tunachojivunia kwenye tamasha la mwaka huu tutaweza kuwaonyesha jinsi ile dawa ilivyotengenezwa,” amesema Ngereza aliyesema wazee wa Kingoni watafanya maonyesho hayo.

Zaidi, Maadhimisho haya yataambatana na siku ya Wangoni ambayo itaambatana na shughuli mbalimbali zitakazoonyeshwa na wazee wa kabila la Wangoni.

Maonyesho haya yanatoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa bidhaa za kitamaduni kuonyesha bidhaa zao za asili ili kuendelea kutangaza urithi wa Tanzania.


Zinazohusiana


Vita vya Maji Maji ni vita vilivyopiganwa na Watanganyika dhidi ya ukoloni wa Ujerumani kuanzia mwaka 1905 hadi Julai 1905. 

Chimbuko la vita hivyo lilikuwa kiongozi wa kimila, Kinjeketile Ngwale aliyewaaminisha watu kuwa kupitia maji aliyoyatengeneza dawa dhidi ya risasi za Wajerumani akidai risasi hizo zisingewadhuru na badala yake zingeligeuka maji.

Aliishi Ngarambe, Matumbi huko Tanganyika ambayo kwa sasa ndiyo Tanzania. Alinyongwa Agosti 1905 na maafisa wa Ujerumani kwa kosa la uchochezi.

Wadau mbali mbali wa historia wamesema watu kati ya 250,000 hadi 300,000 walipoteza maisha katika vita hiyo ambayo haikuwa ya mafanikio kwa Watanganyika.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW