Idadi ya watalii Tanzania yapaa, kimataifa ikishuka

January 21, 2020 12:31 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Idadi ya watalii wa kimataifa imepungua kutoka asilimia 6 mwaka 2018 hadi asilimia 4 mwaka jana.
  • Iidadi ya watalii walioingia nchini Tanzania imeongezeka kutoka milioni 1.3  mwaka 2017 hadi kufikia watalii milioni 1.5 mwaka juzi.
  • Kushuka kwa watalii wa kimataifa kumesababishwa na kudidimia kwa uchumi.

Dar es Salaam. Wakati idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania ikiongezeka, idadi ya watalii ilimwenguni imepungua kutoka asilimia 6 mwaka 2018 hadi asilimia 4 mwaka jana, ikichagizwa na kudidimia kwa uchumi wa dunia. 

Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 kinaeleza kuwa idadi ya watalii walioingia nchini Tanzania imeongezeka kutoka milioni 1.3  mwaka 2017 hadi kufikia watalii milioni 1.5 mwaka juzi. 

Ongezeko hilo limechangia kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka Dola za Marekani bilioni 2.2 (takriban Sh5.1 trilioni) mwaka 2017 hadi kufika Dola za Marekani bilioni 2.4 (takribani Sh5.5 trilioni) mwaka juzi.

Hata hivyo, ripoti ya idadi ya watalii wa kimataifa (World Tourism Barometer) ya mwaka 2020 iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) imebainisha kuwa idadi ya watalii ulimwenguni imekuwa ikishuka kwa miaka mitatu mfululizo tangu mwaka 2017.

Mwaka 2017 idadi ya watalii iliongezeka kwa asilimia saba lakini mwaka uliofuata ikashuka hadi asilimia sita kabla ya kushuka zaidi hadi asilimia 4 mwaka jana hadi watalii bilioni 1.5. 

Kwa mujibu wa shirika hilo, kushuka huko kwa watalii ulimwenguni kumesababishwa na kudidimia kwa uchumi wa dunia, mivutano ya kikanda na hatua ya Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya (Brexit). 

Lakini katika siku zijazo, sekta ya utalii duniani inaweza kukua kwa viwango vya juu ikiwa shughuli za uchumi zitaimarishwa. 


Zinazohusiana:


Ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusu hali ya ukuaji wa uchumi duniani, Januari 2020  inaonyesha kwamba uchumi wa dunia bado unasuasua ingawa ni wenye utulivu baada ya kushuka kwa miaka miwili mfululizo.

“Tumeona ishara zenye kuonyesha kuwa ukuaji wa uchumi ulimwenguni unaweza kuwa umetulia katika viwango fulani. Tunatarajia ukuaji wa uchumi kutengamaa kwa wastani kutoka asilimia 2.9 mnamo 2019 hadi asilimia 3.3 mwaka huu na kisha asilimia 3.4 mnamo 2021,” inaeleza ripoti hiyo ya IMF.

Ukuaji wa idadi ya watalii mwaka 2019 katika bara la Ulaya ulikuwa kwa asilimia 4 huku Asia Pasifiki ukiongezeka kwa asilimia 5 na Afrika uliongezeka kwa asilimia 4. 

Wakati, idadi ya watalii wa kimataifa ikipungua, nchi za Ufaransa, Uhispania na Marekani zimerejea katika nafasi ya juu kwa mara nyingine tena na kuwa nchi tatu ambazo zimetembelewa zaidi duniani kwa mwaka uliopita. 

Enable Notifications OK No thanks