Tanzania kupanua maghala ya kuhifadhi mafuta

June 1, 2022 11:17 am · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Yatajengwa katika maeneo mbalimbali Tanzania.
  • Itaongeza uwezo wa Tanzania kuhifadhi mafuta.
  • Itasaidia kudhibiti upandandaji wa bei za mafuta.

Dar es salaam. Serikali ya Tanzania imesema iko mbioni kuanzisha hifadhi ya kimkakati ya kutunza mafuta (Strategic Petroleum Reserve)  ili kupunguza changamoto ya uhaba na kupanda kwa bei ya mafuta yanayotumiwa na vyombo vya moto.

Waziri wa Nishati January Makamba aliyekuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo (Juni, 1, 2022) amesema Serikali imeendelea kufanya juhudi mbalimbali katika kuhakikisha mafuta yanakuwepo nchini wakati wote.

Uanzishwaji wa hifadhi hiyo ni muhimu ili kuwezesha usalama na uhakika wa upatikanaji wa mafuta wakati wote, ambapo amesema sekta binafsi itashirikishwa katika mpango huo. 

“Kama sehemu ya maandalizi Serikali kupitia TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) inayo tayari maeneo mbalimbali kwa sababu hii hifadhi ya kimkakati haipo eneo moja tu nchini inatawanywa maeneo mbalimbali,” amesema Waziri Makamba ambaye ni mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga.

Makamba hajasema chochote kuhusu uwezo wa hifadhi hiyo katika kuhifadhi mafuta lakini kama utakamilika utasaidia kuongeza uwezo wa Tanzania kuhifadhi mafuta mengi kwa wakati mmoja na hivyo kupunguza haja ya kuagiza bidhaa hiyo kila mwezi kama inavyofanyika sasa. 

Kwa mujibu wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura),  Tanzania Bara ina ghala 22 za kupokelea mafuta zilizopo katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, zenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo milioni 1.3.

 Ghala hizo hupokea bidhaa za petroli kutoka melini. Aidha, kuna ghala 29 nchi kavu, zenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 75,625. 

“Hata hivyo, ghala hizo, nyingi hazifanyi kazi. Pia, Kampuni ya Bomba la Mafuta la TAZAMA inapokea mafuta ghafi kupitia boya (SBM) na kuhifadhi bidhaa hizo kwenye ghala lake lenye mita za ujazo 232,000,” imeeleza Ewura katika tovuti yake.

Baadhi ya mapipa makubwa ya kuhifadhia mafuta katika ghala la kuhifadhi na kupokea mafuta la kampuni ya GBP mkoani Tanga. Aliyekuwa Waziri wa Nishari, Dk Medard Kalemani, alifanya ziara katika eneo hilo, Mei 10, 2020. Picha| Mtaa kwa Mtaa Blog.

Mpango huo kabambe umekuja wakati dunia ikishuhudia kupanda kwa bei ya mafuta kulikochangiwa na vita ya Urusi na Ukraine, jambo lililosababisha kuyumba kwa mifumo ya usafirishaji wa bidhaa hiyo muhimu. 

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imetoa ruzuku ya Sh100 bilioni iliyosaidia kupunguza bei ya petroli na dizeli kwa mwezi Juni, licha ya watumiaji kutaka bei ziendelee kushuka kwa sababu zimepanda kwa kiwango cha juu.

Waziri Makamba amesema katika mwaka wa fedha 2022/23,  wizara yake imeomba Bunge kupitisha kiasi cha Sh2.9 trilioni ambapo moja ya vipaumbele ni kuimarisha mfumo wa uagizaji na uingizaji wa mafuta nchini.


Kamati yaja na maoni yake

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula amesema licha ya kuwepo kwa akiba ya mafuta ya kutosha bado bei imeendelea kupanda hivyo kuwawebebesha mzigo wananchi.

“Upandaji wa bei ya mafuta umekuwa ukichochea kupanda kwa maisha kutokana na bei za bidhaa na utoaji huduma kupaa.” amesema Mbunge huyo wa Mkinga.

Amesema kamati yake inaona njia rahisi ya kutatua changamoto za kupanda kwa bei ya mafuta ni kupunguza utitiri wa kodi katika bidhaa hiyo.


Soma zaidi:


Bidhaa zingine zishuke

Baadhi ya Wabunge wakichangia bajeti hiyo ya Wizara ya Nishati wameipongeza Serikali kwa kutoa ruzuku lakini wameishauri kuchukua hatua madhubuti kumaliza tatizo la uhifadhi na bei za mafuta nchini.

“Tumeona tangu jana usiku mafuta yameshuka imepunguza, angalau makali yale abayo watanzania walikuwa wanayapata hongera sana serikali yetu,” amesema Mbunge wa Kasulu Vijijini, Augustine Holle.

Hata hivyo, Mbunge wa Tabora Mjini, Emanuel Mwakasaka amesema kushuka kwa bei ya mafuta kuende sambamba na kushuka kwa bidhaa zingine ikiwemo vyakula ambavyo zimekuwa zikichangia ugumu wa maisha.

“Wakati wa mafuta yamepanda bei na vitu vingi vipanda bei kwa kisingizio cha haya mafuta…..sasa vitu tuvione vinaanza kupungua bei kama vitu mitaani vitazidi kuwa na hali ile ile wananchi hawawezi kuona unafuu wa kupungua bei ya mafuta,” amesema Mbunge wa Tabora Mjini Emanuel Mwakasaka.

Enable Notifications OK No thanks