“Startups” nne Zanzibar zapenya shindano la Seedstars

August 19, 2019 7:38 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Zimechaguliwa kuingia katika shindano la dunia la Seedstars World likaloziwezesha mshindi kupata mtaji wa Dola za Marekani milioni 1 (Sh2.3 bilioni).
  • Kampuni hizo ni  Nyumbani Care, Zanzibar Health Innovation, Drone Wings na Zanzibit.
  • Kampuni itakayoshinda itapata fursa ya kushiriki mkutano Seedstars nchini Switzerland. 

Dar es Salaam. Kampuni nne za teknolojia zinazochipukia ikiwemo ya Nyumbani Care za Visiwani Zanzibar zimechaguliwa kuingia katika shindano la dunia la Seedstars World likaloziwezesha mshindi kupata mtaji wa Dola za Marekani milioni 1 (Sh2.3 bilioni) na tuzo zingine za uwekezaji. 

Shindano hilo linaendeshwa na kampuni ya ujasiriamali wa teknolojia na uwekezaji ya Seedstars ya nchini Switzerland ambayo ina matawi katika majiji mbalimbali duniani likiwemo Dar es Salaam. 

Kampuni changa (startups) zingine ni pamoja na Zanzibar Health Innovation, Drone Wings na Zanzibit ambazo zimekuwa zikitumia teknolojia kutoa huduma na bidhaa ili kutatua changamoto za jamii. 

Taarifa ya Seedstars iliyotolewa leo (Agosti 19, 2019) imeeleza kuwa kampuni hizo nne zimepatikana baada mchujo uliofanywa kwa kampuni 10 zilizowasilisha mawazo yao bunifu mbele ya majaji. 

Kampuni hizo nne zitashindanishwa na kampuni zingine jijini Dar es Salaam ili kumpata mshindi wa jumla wa Tanzania atakayepata tuzo na msaada wa uwekezaji ili kuifanya biashara yake kuwa endelevu. 

Lakini pia kampuni itakayoshinda itapata fursa ya kushiriki katika mkutano mkuu wa Seedstars utakaofanyika Switzerland hapo baadaye. 

Kampuni zingine sita zilizoshiriki katika mchujo huo ni pamoja na Mjasiri Hub, HI Local Incubator, Sparkle Company, Alis Decoration, Samem Agri Spices na NOPOVO. 


Soma zaidi:


Kituo kitakachofuata cha ziara ya wawakilishi wa Seedstars kitakua Dar es Salaam katika tawi lake la Seedspace ambapo mshindi atakaeiwakilisha Tanzania atapatikana. 

Seedstars imekuwa akitafuta kampuni zinazochipukia zinazotatua changamoto za Afrika kwa kutumia teknolojia na kutengeneza bidhaa zinazokidhi soko la kimataifa ili kuziwezesha kwa mtaji na mafunzo ya uwekezaji. 

Siri ya kampuni zilizoshinda kutoka Zanzibar

Kampuni ya Zanzibar Health Innovation imekuwa ikitengeneza vifaa kwa ajili ya wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo. Drone Wings yenyewe inatumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drones) kutoa mafunzo, kukusanya data na kufanya uchambuzi wa njia sahihi za kusimamia mazingira na kutatua changamoto za jamii. 

Zanzibit imetengeneza mfumo wa programu tumishi ya simu (App)  unaowawezesha watumiaji kuweka miadi na daktari. Nayo Nyumbani Care wametengeneza tovuti na jukwaa la mtandaoni linalowaunganisha wanawake waliopo makazini na wafanyakazi wa nyumbani (house maids). 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW