Somo la kompyuta lawatoa jasho kidato cha sita, Kiswahili chawabeba
- Ufaulu wa somo la kompyuta umeshuka kwa zaidi ya asilimia 20.
- Wadau wasema huenda ni ufundishwaji wa somo hilo kwa nadharia badala ya vitendo.
- Washauri walimu kuwa wabunifu katika ufundishaji.
Dar es Salaam. Wakati ulimwengu ukijipambanua kwa teknolojia ya mawasiliano na matumizi ya kompyuta, huenda sekta ya elimu ya Tanzania inahitaji kuwekeza zaidi katika fani ya teknolojia ili kupata wataalam wengi.
Hilo linatokana na matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2021 yaliyotangazwa Julai 10 kuonyesha kuwa wanafunzi wamefeli zaidi katika somo la sayansi ya kompyuta kuliko masomo mengine.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), ufaulu wa somo la sayansi ya kompyuta umeshuka ufaulu kwa asilimia 26.2 hadi asilimia 60.5 mwaka 2021 kutoka asilimia 82 mwaka jana.
Kiwango hicho cha ufaulu kiko chini kuliko masomo yote ambayo wanafunzi walifanyia mtihani Mei mwaka huu.
Somo la kompyuta limekuwa likifundishwa shuleni ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa kutumia programu na mifumo ya kifaa hicho ambacho kimekuwa kiungo muhimu kwa shughuli za maendeleo haya zile zinazofanyika kwa njia ya mtandao (intaneti).
Mbali nakusumbuliwa na somo la kompyuta, masomo mengine yaliyowatoa jasho wanafunzi katika mtihani huo ni pamoja na somo la hisabati ambalo ufaulu wake ni wa asilimia 60.8 kwa mwaka 2021.
Hata hivyo, ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2020, ufaulu wa somo hilo umepanda kidogo kutoka asilimia 59.3.
Somo lingine lenye ufaulu wa chini ya asilimia 90 ni somo la lugha ya Kiarabu ambalo ufaulu wake pia umeshuka kutoka asilimia 81.8 mwaka jana hadi asilimia 75 mwaka huu.
Licha ya Fizikia, Kemia na Biolojia kuwa sehemu ya masomo ya sayansi pamoja na kompyuta, wanafunzi wamefanya vizuri ambalo kwa kila somo ufaulu uko juu ya asilimia 92.
Baadhi ya wanafunzi wa somo la kompyuta wanashindwa kufaulu kutokana na kusoma somo hilo kwa nadharia. Picha| Borgen Magazine.
Kiswahili chawabeba watahiniwa
Bila shaka kwa baadhi ya wanafunzi chumba cha mtihani kilikuwa ni uwanja wa shangwe kwa mwaka huu ambapo ni masomo matatu tu kati ya masomo 18 yaliyofanyiwa mtihani mwaka 2020 ndiyo ufaulu wake upo chini ya asilimia 90.
Somo ambalo wanafunzi wamefaulu bila kufeli ni somo la Kiswahili ambalo ufaulu wake ni wa asilimia 100. Kwa somo hilo, ufaulu huo ni muendelezo wa mwaka jana ambapo pia hakukuwa na mwanafunzi aliyefeli somo hilo.
Mbali na kiswahili, masomo mengine yenye ufaulu wa juu mwaka huu ni ni Jiografia (asilimia 99.9) na biashara (commerce) lenye ufaulu wa asilimia 99.8. Kiingereza (asilimia 99.7), Historia ni asilimia (99.7) na Uchumi ni asilimia 99.3.
Nini kifanyike kuinua ufaulu wa somo la kompyuta?
Mtaalamu wa masuala ya kompyuta mkoani Dar es Salaam, Jensen Seth amesema ili mwanafunzi wafaulu somo lolote anahitaji kulipenda somo, kuwa na mwalimu mzuri na kulifanya kwa vitendo.
Mfano, kwa somo la Kiswahili, huenda wanafunzi wanafaulu kwa wingi kutokana na somo hilo kwanza kufundishwa kwa lugha ya Taifa na hivyo wanaelewa maswali yanataka nini tofauti na masomo mengine yanayofundishwa kwa lugha ya Kiingereza.
Seth amesema kwa somo kama kompyuta, linakuja na misamiati yake mipya kabisa na hivyo kuhitaji kufanywa kwa vitendo zaidi kuliko nadharia.
“Ukimfundisha mwanafuzi somo la kompyuta kwa michoro ya kitabu tu, ni ngumu kulifanya kwa vitendo pale inapobidi. Pia, sidhani kama miundombinu inatosha kwenye shule za Serikali kwa ajili ya mafunzo ya vitendo. Wanaosoma kompyuta huku wakifanya kwa vitendo ni wachache na wengine hawajawahi kuiona kabisa kompyuta yenyewe,” amesema Seth.
Mtaalamu wa masuala ya kompyuta Rafia Ramadha amesema baadhi ya wanafunzi huingia kwenye maabara ya kompyuta bila walimu na hivyo kukosa msaada wa kitaaluma kwenye somo hilo. Picha| Teaching Times.
Wadau wengine wameshauri walimu wa somo hilo wajengewe uwezo zaidi ili kuwawezesha kufundisha kwa ufanisi wanafunzi.
Mtaalamu wa masuala ya kompyuta ambaye ni Mratibu wa Maudhui kutoka kampuni ya Empower Limited, Mayur Nayi ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kufaulu kwa wanafunzi somo wakati mwingine inategemeana na ufundishaji wa mwalimu.
Amesema Ufaulu unahusiana na jinsi mwalimu anavyohamasisha wanafunzi kupenda somo hilo kwa ubunifu katika ufundishaji wake hivyo huenda walimu wa somo hilo wana jambo la kujifunza kwa matokeo hayo.
“Huenda ni kwa sababu masomo yanachosha badala ya kufurahisha. Kwa somo kama la kompyuta, unatakiwa kulifanya somo la kufurahia ili mwanafunzi apate hamasa ya kulipenda.
“Ukilifanya somo la kufurahia kujifunza, hawatotaka kujifunza tu bali hata kulifaulu pia,” amesema Nayi.
Latest