Siyo kweli: Chanjo ya Uviko-19 inasababisha homa za muda mrefu
- WHO yasema hakuna uthibitisho wa kisayansi kuhusu suala hilo.
- Ni kweli mtu anaweza kupata homa baada ya kupata Uviko-19 ambayo inaweza kudumu kwa vipindi tofauti.
- Wananchi washauriwa kupata chanjo.
Dar es Salaam. Ikiwa wewe ni miongoni mwa watu waliosikia taarifa kuwa chanjo ya Uviko-19 inasababisha homa ya ugonjwa huo kwa muda mrefu, taarifa hiyo siyo ya kweli.
Uzushi huo unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii unasema mtu akichanja chanjo ya Uviko-19 anapata homa ya muda muda mrefu ya ugonjwa huo, jambo ambalo halijathibitishwa na wataalamu wa afya.
Homa hiyo inayozungumziwa inahusisha dalili kama kikohozi cha muda mrefu, uchovu wa viungo vya mwili, kukosa ladha ya chakula, wasiwasi pamoja na msongo wa mawazo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) dalili hizo hazisababishwi na chanjo bali ni hali inayoweza kumpata yeyote aliyewahi kuambukizwa ugonjwa wa Uviko-19.
Dk Janet Diaz, Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa kliniki kutoka WHO aliyekuwa akihojiwa kwenye kipindi cha Science 5, Julai 30, 2021 anasema kupunguza maambukizi ya Uviko-19 na homa za muda mrefu baada ya Uviko (Post Covid and long Covid) ndio njia pekee ya kuondokana na hali hiyo.
“Matumizi ya chanjo tunayojua hupunguza kulazwa hospitalini, hupunguza vifo, na kwa hivyo wale wote wanaostahili wanapaswa kufanya hivyo,” alisema Dk Diaz.
Sambamba na hilo Kituo cha Kinga na Udhibiti wa Magonjwa (CDC) cha nchini Marekani katika taarifa yake iliyotolewa Septemba 1, 2022 kinaeleza kuwa watu wasiopata chanjo ya ugonjwa huo wapo hatarini zaidi kupata homa hizo za muda mrefu.
“Watu wasiopata chanjo ya Uviko-19 wapo kwenye hatari kubwa ya kupata homa za baada ya Uviko -19 ikilinganishwa na watu ambao walichanjwa,” kimesema kituo hicho.
Zinazohusiana:
Homa za muda mrefu ni nini?
Kwa mujibu wa CDC, homa za muda mrefu zinazosababishwa na Uviko-19 ni matatizo ya kiafya yanayorejea au yanayoendelea baada ya mtu kupata Uviko-19.
Mtu yeyote ambaye aliambukizwa anaweza kukumbana na homa hizo, wengi wao hupata dalili siku chache baada ya kujua kwamba walikuwa na Uviko-19 na wengine dalili hizo zinaweza kudumu kwa wiki, mwezi au mwaka.
Dalili za homa hizo zinafanana na zile za maambukizi mapya ya ugonjwa wa Uviko-19.
Hata hivyo, taarifa hiyo kutoka CDC inasema hakuna kipimo cha kutambua homa za muda mrefu. Watu wanaweza kuwa na dalili mbalimbali ambazo zinaweza kutokana na matatizo mengine ya kiafya.
“Mtoa huduma wa afya anachoweza kufaya ni kuchukua vipimo na kufuatilia hali ya afya ikiwa ni pamoja na kama mgonjwa aliwahi kupata virusi vya ugonjwa huo kabla,” inaeleza taarifa hiyo.
Sambamba na hayo wataalamu wa afya kutoka WHO akiwemo Dk Diaz wanasema ni vyema kupata ushauri wa daktari endapo utahisi dalili hizi za muda mrefu ili kujihakikishia usalama wa afya yako.
Dalili nyingine hazitaisha kwa muda mfupi, hata zikiisha bado mgonjwa anashauriwa kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.
Latest
