Siri Mtanzania kupanda mlima Kilimanjaro mara 300
- Ni Harlod Mndewa, muongoza watalii katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
- Alipanda kwa mara ya kwanza mwaka 1999.
- Umbali aliotembea kupanda mlima ni zaidi ya safari ya kutoka Dar es salaam mpaka Kigoma.
Dar es Salaam. Inawezekana ukawa miongoni mwa watu wachache waliosikia habari za Mtanzania aliyeweka rekodi ya kupanda mlima Kilimanjaro mara 300 na kuwa na shauku ya kufahamu namna gani alifanikisha jambo hilo.
Ni Harlod Mndewa, muongoza watalii katika Hifadhi za Taifa ya Mlima Kilimanjaro na Ngorongoro.
Harlond ameweka rekodi ya kutembea jumla ya kilomita 1,768 kwa kupanda umbali wa mita 5,895 kufikia kilipo kilele cha mlima Kilimanjaro mara 300, umbali ambao ni zaidi ya safari ya kutoka Mkoa wa Dar es salaam mpaka Kigoma.
Safari ya kwanza mlimani
Rekodi hiyo haikufikiwa kwa bahati mbaya bali ni jitihada za makusudi alizoanza miaka 23 iliyopita, baada ya kuamua kuifanya shughuli ya kuwaongoza watalii kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika kama kazi yake rasmi ya kumuingizia kipato baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
“Kwa mara ya kwanza nimepanda mlima mwaka 1999 baada ya kumaliza kidato cha sita, sikupata matokeo ya kwenda chuo kikuu ikabidi nianze tu kutafuta maisha. Kwa hiyo nilianza kupanda kama mpagazi,” anasema Harold.
Kutokana na kazi aliyoichagua Harold alilazimika kujifunza vitu vingine vya ziada ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi ikiwa ni pamoja na kujifunza kupika na kuwaoongoza watalii kupanda milima.
Miaka michahe baadaye akaamua rasmi kwenda kusomea taaluma ya kuongoza watalii ambako alijifunza vitu vingi zaidi kama ikolojia, huduma kwa watalii, huduma ya kwanza pamoja na jiolojia.
Harlod Mndewa, muongoza watalii katika Hifadhi za Taifa ya Mlima Kilimanjaro na Ngorongoro akiwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Picha | Harlod Mndewa.
‘Mikasa mlimani’
Harlod ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kupanda mlima mara 300 kumemkutanisha na mikasa mingi lakini ule uliomtia simanzi ni aliposhuhudia raia wa kigeni akipoteza maisha mbele yake.
“Hakuwa mgeni wangu alikuwa wa “mtu mwingine, nahisi kulikuwa kuna uzembe fulani ulitokea kwa kweli tukio lile huwa nakumbuka kila siku,” anasema Harlod.
Tukio hilo halikumfanya asite kuendelea kuongoza wageni kupanda Mlima Kilimanjaro bali aliendelea akiwa makini zaidi mpaka alipofikisha safari 300.
Soma zaidi:
-
Kwa nini mchango wa sekta ya misitu ni mdogo katika pato la Taifa?
-
Mapato sekta ya utalii yapaa Tanzania
Safari 300 siyo bure
Safari hizo ni sehemu ya kazi yake ya kuongoza watalii, hivyo amekuwa akijipatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yake.
“Kwanza imenipa heshima kwa kutunza rekodi watu wanapanda tu hawaweki rekodi. Pili nimeisaidia nchi yangu kupata mapato, imenikutanisha na watu na naendesha maisha yangu kupitia kazi hii,” anasema Harold ambaye ni mume na baba wa watoto watatu.
Pia kumeimarisha zaidi afya yake kwani ni miongoni mwa mazoezi mazuri kwa mtu yoyote akifafanua kuwa kwa wale wanaotaka kupunguza uzito basi kwa kupanda Mlima Kilimanjaro unaweza kupunguza kati ya kilo nne mpaka sita.
Hata hivyo Harold amesema zipo baadhi ya changamoto ambazo anaamini zikifanyiwa kazi zinaweza kuikuza zaidi sekta ya utalii.
Changamoto hizo ni pamoja kuboreshwa kwa maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya utalii wakiwemo madereva na waongoza watalii kwani hao ndiyo wanaofanya kazi kubwa kuisemea vizuri nchi.
“Mimi ndiye ninakaa na mgeni kwa siku zote anazokuwepo hifadhini, namhudumia na kuhakikisha anaondoka na picha nzuri ya nchi yetu lakini tunachopata hakiendani na kazi tunayofanya,” anasema Harold
Gharama kubwa za viingilio pamoja na miundombinu ya utalii ni miongoni mwa changamoto nyingine ambazo Harold anaamini zinatakiwa kutupiwa macho kwa ukaribu na kufanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, utalii huchangia asilimia 25 ya fedha za kigeni na huzalisha ajira takriban milioni 1.6 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa mwaka.
Muongoza watalii, Harlod Mndewa akiwa na wateja wake wakati wakiendelea na safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro. Picha | Harlod Mndewa.
Jitokezeni kupanda Milima Kilimanjaro
Harold amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuupanda Mlima Kilimanjaro kwani si kazi ngumu kama inavyodhaniwa ambapo amewashauri kujiunga kuanzia watu wanne na kuendelea ili kupunguza gharama ambapo kwa Mtanzania mmoja atapaswa kulipa kuanzia Sh1.2 milioni.
Usikose sehemu ya pili ya makala haya itakayoelezea mambo ya kuzingatia wakati wa kupanda Mlima Kilimanjaro na faida zake.